UKURASA WA 943; Usiendeshwe Na Hofu Kwenye Maamuzi Haya…

By | July 31, 2017

Hofu ni kinyume cha upendo, huwezi kuwa na upendo na hofu kwa wakati mmoja. Ni labda upende kitu na ukifanye kwa mapenzi, au uwe na hofu na ukifanye kwa kusukumwa na hofu.

Wote tunajua kwamba tunafanya kitu kwa ubora pale tunaposukumwa na mapenzi na siyo hofu.

Hivyo basi;

Kama sababu pekee inayokusukuma ufanye kitu ni hofu ya utaonekanaje usipofanya, usikifanye.

Kama sababu pekee inayokusukuma kufanya kitu ni kuhofia kujutia baadaye kwa kutokufanya, usifanye.

Kama sababu peke inayokusukuma ufanye kitu ni hofu kwamba usipofanya kuna kitu utakosa, usifanye.

Usifanye chochote ambacho kinatokana na hofu, hayatakuwa maamuzi sahihi kwako na una nafasi kubwa ya kukosea.

Badala yake fanya maamuzi kutokana na upendo, mapenzi yako juu ya kitu husika.

Fanya kitu kwa sababu unapenda kufanya, kwa sababu unajua unatoa mchango mkubwa. Na siyo kwa kusukumwa na hofu, hofu haitakusaidia lolote.

SOMA; Njia Nyingine Ya Kuishinda Hofu Ni Hii…

Kama unaanzia kwenye hofu, basi unahitaji kuanza kubadili mtazamo wako na kwenda kwenye upendo. Kwa mfano kama sababu pekee inayopelekea wewe ufanye kazi yako ni hofu kwamba utashindwa kuendesha maisha yako, anza kubadili mtazamo wako na kuangalia eneo lipi la kazi unayoifanya ambalo unalipenda. Angalia ni mchango gani unatoa kwa wengine, angalia unajisikiaje pale unapokamilisha jukumu fulani. Hii itakusaidia kuanza kufanya maamuzi bora na sahihi kwako.

Hama kwenye hizo hofu ambazo umejijaza, haziwezi kukufikisha kwenye mafanikio, kwa sababu hofu mara zote inakuharakisha kufanya mambo, na hakuna jambo lolote zuri limewahi kufanywa kwa kuharakishwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.