UKURASA WA 947; unapopata shida ya kuamka asubuhi, jikumbushe hili…

By | August 4, 2017

Usingizi ni mtamu, lakini pia usingizi huwa hauishi, upo kila siku. Kuna wakati muda wa kuamka unakuwa umefika lakini hujisikii kabisa kuamka. Labda umeweka kengele ya kukuamsha, kengele hiyo inapiga lakini unajiambia unalala dakika tano tu utaamka. Unakuja kuamka nusu saa au hata saa nzima baadaye na kuwa umechelewa kuanza mipango yako ya siku.

Kupata shida ya kuamka asubuhi inaweza kusababishwa na mengi. Inaweza kuwa ni uchovu kutokana na kazi ngumu za siku iliyopita, au kuchelewa kulala na hivyo kukosa usingizi wa kutosha. Lakini pia inaweza kutokana na kukosa hamasa ya kile unachofanya. Kwa mfano kama unafanya kazi au biashara ambayo huipendi, kuamka asubuhi kunakuwa shida kwako. Kila ukikumbuka ni siku nyingine ya kwenda kwenye kitu ambacho hukipendi, unakosa kabisa hamasa ya kuamka.

Lakini pamoja na yote hayo, hatuwezi kuendelea kulala, hata kwa dakika moja, hasa kama tumeshajitoa kwa ajili ya mafanikio. Tunahitaji kuamka kwa wakati, iwe tumechoka au la, iwe tuna hamasa au hatuna.

SOMA; Angusha Na Tawala Watu Hawa Wawili Ili Uweze Kuwa Na Mafanikio Makubwa.

Swali ni je tunawezaje kujisukuma kuamka asubuhi kama hatujisikii kufanya hivyo? Nimekuwa nakushirikisha njia mbalimbali za kupata hamasa ya kuamka asubuhi. Leo nimejifunza njia nyingine inayoweza kuwa bora kabisa kukupa hamasa ya kuamka mara moja na kuacha kuendelea kulala.

Njia hiyo ni kuwafikiria wanyama. Sisi na wanyama wote tunalala, lakini sisi binadamu tuna kitu cha pekee cha kututofautisha na wanyama. Mnyama analala kutokana na hali ilivyo, giza limeingia analala, giza likiisha anaamka. Na anapoamka lengo lake kuu ni kupona, hivyo aweze kupata chakula na wakati huo huo aepuke vitu vinavyohatarisha maisha yake, kama wanyama hatari na hali hatari.

Lakini sisi binadamu tuna tofauti na wanyama, kwa sisi tuna madhumuni makubwa zaidi ya maisha zaidi tu ya kuwa hai. Sisi tuna uwezo wa kuyafanya maisha yetu na ya wengine kuwa bora zaidi, kupitia shughuli mbalimbali tunazofanya. Na hivyo asubuhi inapofika, tujikumbushe kwamba ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu ya kwenda kutoa mchango bora kwa wengine.

Hata kama tunachofanya hatukipendi kwa sasa, tukumbuke kuna watu kinawasaidia, wapo watu ambao maisha yao yanakuwa bora kupitia sisi. Na hawa ndiyo wanapaswa kukupa wewe hamasa ya kutokupoteza hata dakika moja kitandani.

Na kama hilo bado halikupi hamasa ya kuondoka kitandani, jiulize je kwa kuendelea kulala, unajitofautishaje na ng’ombe? Hata ng’ombe anaweza kulala, lakini kuamka kwake siyo kwa maamuzi makubwa kama yako. Jitofautishe na ng’ombe kwa kufanya maamuzi muhimu ya maisha yako.

Hili litakuwezesha wewe kuweza kujidhibiti kwenye muda wa kuamka na kuweza kuanza siku yako kulingana na mipango yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

2 thoughts on “UKURASA WA 947; unapopata shida ya kuamka asubuhi, jikumbushe hili…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.