UKURASA WA 948; Uongozi Ni Kujali…

By | August 5, 2017

Kwanza kabisa, wote wanaofanikiwa na kuweza kufanya mambo makubwa, ndani yao wana sifa za uongozi, iwe kwa mazoea au kujijengea, huwa ni viongozi wazuri sana.

Ninaposema kiongozi simaanishi yule tu aliyechaguliwa na kupewa jina hilo, bali yeyote ambaye anachukua hatua ya kufanya mambo kuwa bora zaidi.

Hivyo basi, kila mmoja wetu anapaswa kuwa kiongozi bora, ili kuweza kuwa na maisha ya mafanikio.

Ni sifa moja ya viongozi bora ni kujali, jali sana kile unachofanya na jali wale wote wanaokuzunguka, na mambo yako yatakuwa mazuri popote pale ulipo.

Uongozi unaanzia kwenye ngazi ya familia, kwa yeyote ambaye ni wa karibu kwako, awe ndugu, mwenza, watoto, wazazi, unapowajali unafanya maisha yao kuwa bora zaidi, unawawezesha nao kuwa bora zaidi.

SOMA; Sifa Kuu Ya Uongozi Unayotakiwa Kuwa Nayo…

Uongozi pia unahusika kwenye kazi yoyote mtu anayochagua kufanya, hata kama ni ndogo kiasi gani, unapojali kuhusu yule anayepokea kile unachofanya, unakifanya kwa ubora, unayafanya maisha yao kuwa bora na kukuthamini sana. Unapojali kuhusu wale unaofanya nao kazi, mahusiano yenu yanakuwa bora, ushirikiano unakuwa mkubwa na wote mnanufaika.

Kwenye biashara ndiyo kabisa uongozi unahitajika sana, tena sana. Kuweza kuwapa wateja wako huduma nzuri, lazima uwajali, lazima ujitoe hasa kuhakikisha wanapata kilicho bora. Kuweza kupata wasaidizi bora lazima uwajali na kupitia hilo mnaweza kushirikiana vizuri na kufanya kazi bora.

Hakuna uongozi kama hakuna kujali, hivyo kwa vyovyote vile, tanguliza kujali maslahi ya watu wengine kabla hujaanza kuangalia maslahi yako binafsi. Simaanishi ujinyime, lakini usijiangalie wewe mwenyewe na kusahau kwamba wengine nao wana mahitaji yao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.