UKURASA WA 950; Ona Mwisho Kabla Hujaanza Safari…

By | August 7, 2017

Watu wengi huanza safari, bila ya kujua safari hiyo wanaelekea wapi, na hata kama wanajua, hawauoni ule mwisho wa safari ambayo wanakuwa wameianza. Na hata kama siyo mwisho, basi hawaoni njia ya safari hiyo ipoje.

Hivyo wanajikuta wakizunguka tu wasijue wapi wanafika, wanakazana sana lakini hawaendi mbali. Ni sawa na mtu aliyepotea njia, halafu yupo kasi kweli kweli, anakazana kuongeza mwendo afike haraka, huku tayari amepotea.

Fikiria mtu anayefanya kazi ambayo anachowaza yeye ni ule mshahara anaoupata tu. Hafikirii kitu kingine, yeye anaichukulia kazi hiyo kama sehemu ya kuendesha maisha yake. Kwa namna hiyo hawezi kuweka juhudi kubwa, wala hawezi kuwa na ubunifu mkubwa. Kwa sababu yeye anachowaza ni kile anachopata na hawezi kuweka juhudi kwa sababu hapati kama anavyotaka yeye. Hawa ndiyo utawasikia wakisema, kwani wananilipa kiasi gani mpaka nijitese kiasi hicho? Kwa maelezo kama hayo au yanayofanana na hayo, unajua kabisa mtu hana maono yoyote makubwa kwenye kazi hiyo wala maisha yake.

SOMA;  Hatua Iliyo Ngumu Zaidi Kwenye Safari Ya Mafanikio…

Hivyo pia kwenye biashara, tunaona wafanyabiashara wengi wapo pale pale, wakifanya biashara ndogo. Biashara zipo pale pale miaka yote, hazikui wala kuwa bora zaidi. Wao wanachochukulia ni kwamba biashara ni sehemu ya kutengeneza fedha ya matumizi. Hivyo kila wanachopata wanatumia. Hawana picha nyingine tofauti ya kibiashara, hakuna maono ambayo wanayafanyia kazi. Na hilo linakuwa kikwazo kikubwa kwa biashara zao kukua.

Rafiki yangu, kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kwanza una maono makubwa ya hicho unachofanya. Jione ukiwa mbali zaidi, ukifanya makubwa zaidi. Maono haya jikumbushe kila siku, na hilo litakusukuma wewe kufanya zaidi ya kawaida. Litakuonesha wewe fursa za kuwa bora zaidi na utaweza kufanya kwa utofauti zaidi.

Kama huoni mwisho wa safari yako, kama huoni jinsi safari hiyo inavyokwenda, usikazane kuweka kasi, kwa sababu haitakufikisha popote. Badala yake kaa chini na pata picha ya safari yako upya, ili unapoweka kasi, iwe sahihi na ilete matokeo bora na yatakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.