UKURASA WA 960; Usiishi Kwenye Hali Ya Haraka Kila Wakati…

By | August 17, 2017

Mwanafalsafa mmoja amewahi kunukuliwa akisema maisha ni kile kinachotokea wakati sisi tunakazana kufanya mambo mengine. Akiwa na maana kwamba, mengi tunayokazana kufanya siyo yanayotengeneza maisha yetu, bali vile tunavyoenda ndivyo tunavyotengeneza maisha yetu. Kwa bahati mbaya sana, huwa tunakazana na yale tunayofanya na kusahau kabisa vile tunavyoenda.

Ndiyo maana mtu anaweza kuwa anakazana na kazi, akasahau afya yake, anakuja kustuka hali ya afya ni mbaya na hawezi kwenda tena na yale aliyokuwa anakazana nayo.

Tunaishi kwenye dunia ya haraka, tunaweza kusema dunia ya mwendokasi. Watu hawana subira tena. Tafiti zinasema mtu akifungua ukurasa wowote mtandaoni na ukachukua zaidi ya sekunde sita kufunguka, anaachana nao na kuendelea na mambo mengine.

Tunataka kila kitu kitokee sasa, na kitokee kwa haraka sana. Hatuna kabisa muda wa kusubiri. Hili linatugharimu sana kuishi maisha ya mafanikio.

Kwa sababu kadiri tunavyokazana kwenda haraka, ndivyo tunavyoyakimbia maisha yetu. Kwa mfano mtu anayekula haraka ili awahi mambo mengine, hawezi kukifurahia chakula. Atakuwa anakula kwa sababu tu inambidi ale, lakini siyo kula kwa sababu anataka kukifurahia chakula.

Jambo moja la kushangaza sana, huwa tuna haraka ya kufanya kitu chenye maana, ili kuwahi kwenda kufanya kitu ambacho hakina maana kabisa. kwa mfano unamhudumia mteja haraka haraka ili aondoke, na wewe upate muda wa kuperuzi simu yako, kuingia kwenye mitandao ya kijamii au kupiga soga na wengine.

Tunafanya hivi kwenye kazi na hata mahusiano yetu. Ni vigumu sana zama hizi kukuta watu wamekaa wakiongea, kwa muda hata wa nusu saa tu kabla kila mtu hajaanza kutumia simu yake. Watu watakazana kufanya mambo haraka haraka kama vile kuna sehemu muhimu sana wanayowahi, halafu wanaishia kufanya mambo ambayo hayana umuhimu wowote.

SOMA; Kirusi Kinachoua Ndoto Za Wengi Kwa Haraka…

Hivyo wito wangu kwetu wanamafanikio wote, tuache kuishi kwa haraka, hasa kwa yale mambo ambayo ni muhimu zaidi kwetu. Tuweke vipaumbele vya maisha yetu, tutenge muda wa kutosha kwenye kila kipaumbele, kisha tufanye kile ambacho tumepanga kufanya, kwa utulivu kabisa, bila ya kuwa na haraka yoyote ile. Tufanye kitu kwa manufaa ya kitu kile, kwa kile ambacho tunapata kutoka kwenye ufanyaji wa kitu husika. Na siyo tufanye kwa sababu tunataka kumaliza na kwenda kwenye kitu kingine.

Wakati unachaga kufanya kitu kimoja, hakuna tena kitu kingine muhimu zaidi ya kile ulichopanga kufanya. Mwili wako, akili yako na hata mawazo yako yote yanapaswa kuwa pale.

Tumalize na adui mkubwa wa zama hizi..

Simu janja au kama zinavyojulikana kwa kiingereza ‘smartphone’.

Kama kwenye siku yako, huwezi kukaa mbali na simu yako hata kwa nusu saa pekee, huna maisha. Ndiyo nasema kwa herufi kubwa kwamba HUNA MAISHA. Kwa sababu muda wote una usumbufu, huwezi kufanya kitu kimoja, ukaweka akili yako yote pale. Kila baada ya dakika chache utaingia ujumbe, itaingia simu, na sumu zaidi, utataka kuingia mtandaoni uone unapitwa na nini.

Lazima tuweze kudhibiti adui huyu anayewamaliza wengi. Lazima tudai muda wetu, muda wa kukaa na kufanya kazi zetu kwa utulivu, muda wa kukaa na kuongea na mtu, ana kwa ana, bila ya kuhamia kwenye simu. Lazima tudai muda wetu wa kutuliza akili na mawazo yetu, bila ya kukimbilia kwenye simu zetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 960; Usiishi Kwenye Hali Ya Haraka Kila Wakati…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.