UKURASA WA 965; Kufanya Vitu Kwa Usahihi Na Kufanya Vitu Sahihi…

By | August 22, 2017

Kwanza kabisa, watu hawapendi kujisumbua, hawapendi kuumiza vichwa vyao kufikiria mambo magumu. Ndiyo maana kila siku utaona watu wanakazana kufanya mambo rahisi, mambo yaliyozoeleka.

Na matapeli nao wanatumia fursa hiyo kuwatapeli wengi, kwa kuwaonesha kwamba ipo njia rahisi ya kupata makubwa wanayotaka. Wakati ukweli ni kwamba njia ya aina hiyo haipo, na haijawahi kuwepo.

Sasa leo nataka tujadili kwa kina kuhusu kufanya vitu kwa usahihi na kufanya vitu sahihi.

Watu wengi hukazana sana kufanya vitu kwa usahihi, kwa namna wengine wanavyofanya. Na wakati mwingine wanakazana hata zaidi ya wengine. Lakini wanapofika kwenye kile wanachokazana kufikia, wanagundua kwamba hakikuwa kitu sahihi kwao kufanya. Ndiyo wamefanya kwa usahihi kabisa, lakini hakikuwa kitu sahihi.

SOMA; Ongea Unavyotaka, Lakini Watu Watasikia Wanachotaka Kusikia…

Ni sawa na kutafuta ngazi, kuiweka ukutani, kukazana kupanda, halafu unafika juu na kugundua kumbe ngazi yenyewe hukuiweka kwenye ukuta sahihi. Ndiyo juu umefika, lakini siyo sehemu sahihi kwako kuwepo.

Watu wengi wamekuwa wakigundua hilo muda ukiwa umeshapita, wanakuwa wameshawekeza muda mwingi na nguvu pia kufanya kitu kile kwa usahihi, kiasi kwamba hata baada ya kugundua siyo kitu sahihi kwao, inabidi waendelee nacho pekee.

Na hii inasababishwa na tabia ya watu kukazana kufanya kile walichozoea kufanya, na kukosa muda wa kutafakari na kujihoji kila siku juu ya kule wanakokwenda na yale wanayofanya.

Watu wanajisahau wao wenyewe na wanapotezwa na kelele za dunia, pamoja na mbio zao wenyewe, mpaka pale wanapofika ukingoni ndiyo wanakuja kuona ukweli ambao walipaswa kuuona muda mrefu mno.

Leo chukua muda wa kukaa na kutafakari kwenye kila kitu unachofanya. Jiulize je unafanya kitu sahihi kwako au unafanya kitu kwa usahihi. Angalia kila unachofanya, pata picha ya matokeo utakayoyapata, kisha angalia kusudi la maisha yako na maono makubwa uliyonayo kwenye maisha. Je vitu hivyo vinaendana, je kila unachofanya kila siku, kitakufikisha kwenye yale maono makubwa uliyonayo?

Wakati mwingine watu wanakuwa na kitu sahihi wanakifanya, kinachoendana na maono yao na kusudi la maisha yao. Lakini biashara za maisha ya kila siku zinawapoteza na kujikuta wamesahau njia sahihi kwao na kuhangaika na mambo ambayo siyo sahihi.

Ni muhimu kujikumbusha hili kila siku, ili pale unapojikuta unakazana na vitu ambavyo siyo sahihi, uweze kurudi kwenye njia yako na kujali vile ambavyo ni muhimu na sahihi.

Wanasema hakuna maana ya kwenda kasi kama umepotea njia. Lakini unapoangalia namna wengi wanavyoenda kasi kwenye njia zisizo na mwisho mzuri, ndiyo unagundua watu hawapendi kujifunza kutoka kwa wengine. Kabla hujaendelea na kasi za dunia ya sasa, hebu kaa chini na tafakari kasi hizo zinakupeleka wapi.

Kuna kelele nyingi sana zinaendelea huku duniani, kuna ushauri wa kila aina, kuna hofu juu ya hofu, kuna vitisho na kukatishwa tamaa. Iwapo utakuwa hujajua kipi sahihi kwako kufanya na kupambana nacho kukifanya, utajikuta unafanya mambo ya hovyo kwa usahihi, halafu mwisho wa siku huoni kipi kikubwa umekamilisha kwenye maisha yako.

Fanya hili liwe zoezi lako la kila siku, hasa pale unapoamka, pata muda wa kutafakari kila unachofanya, kwa jicho la je ni kitu sahihi kwako kufanya au unafanya tu kwa usahihi.

Matumaini yangu ni kwamba bado hujachelewa, na linapokuja jambo muhimu kwako, hakuna kuchelewa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.