UKURASA WA 967; Mtu Wa Kwanza Kukuangusha Ni Huyu…

By | August 24, 2017

Kwa kuwa unaijua falsafa yangu, hasa kwenye ufanyaji kazi na mafanikio, kabla hata hujafungua kusoma hapa najua utakuwa unajibu tayari, kwamba mtu ninayekwenda kumzungumzia hapa ni wewe mwenyewe. Ila nataka nikushawishi zaidi kwa nini ni wewe na unaepukaje kujiangusha.

Kwa wale ambao hawakuwa wamepata hilo haraka ni kwamba, mtu wa kwanza kukuangusha kwenye maisha yako na kwenye jambo lolote unalofanya au kutaka kufanya, ni wewe mwenyewe. Wewe ndiye wa kwanza kabisa na unaruhusu wengine kukusaidia hilo na ndiyo maana unashindwa kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Lakini utaniambia vipi kuhusu wazazi wangu ambao wameniwekea vikwazo kwenye mengi? Vipi kuhusu mwajiri wangu ambaye ananibana? Vipi kuhusu serikali ambayo inanikamua kodi bila ya kujali udogo wa biashara yangu?

Na yote hayo upo sahihi kabisa, kwamba wapo watu ambao wanachangia kuanguka kwako, kwa namna moja au nyingine, lakini hawa wanachangia tu. Yupo anayeanzisha, ambaye ni wewe mwenyewe. Hivyo wewe umekuwa unaanzisha na kutengeneza kuanguka kwako, halafu wengine wanakusaidia kumalizia anguko hilo. Ila upo vizuri kuwatupia lawama wale wanaochangia tu na kusahau anayeandaa anguko.

SOMA;  Nunua Muda Kwanza….

Kabla hatujaendelea tupate mfano mmoja wa asili, kwa sababu kwenye kila kitu huwa napenda kurudi kwenye asili na kuona asili inaamuaje. Kwa sababu sheria za asili huwa zinafanya kazi bila ya kujali zinafanya kazi wapi na kwa nani. Tuchukue mfano una shamba, ambapo ndani yake una mazao tofauti, una mipapai, una miembe, una minazi na katikati ya shamba una mbuyu mkubwa kabisa. siku moja mvua ikaanza kunyesha, ikiwa na upepo wa wastani, lakini ambao hauishi, unaendelea tu, unafikiri ni zao lipi kati ya hayo litaanza kudhurika na upepo? Jibu lipo wazi, mipapai itaanza kuvunjwa na upepo. Muda unaenda na upepo unazidi kuwa mkali zaidi, hapo miembe itafuatia kuvunjwa matawi. Upepo unaendelea na wakati huu kuna vimbunga kabisa, miembe yote itang’olewa na hata minazi. Lakini katikati ya shamba utabaki mbuyu, ambao kama utasumbuliwa sana, utavunja matawi pekee, shina la mbuyu litaendelea kuwepo.

Sasa hebu niambie hapo, kama shida ni upepo, kwa nini mbuyu usivunjike kama unavyovunjika mpapai? Sijui unapata kile nataka kukuonesha hapa? Kwamba kitu kinaanzia ndani kabla ya sababu za nje kusababisha. Mpapai unavunjika wa kwanza kwa sababu asili yake ni mwepesi ukilinganisha na mbuyu.

Sasa kwa mimea, haina uwezo mkubwa wa kujibadili, lakini sisi binadamu, tunao uwezo mkubwa mno wa kuchagua tuwe mipapai au tuwe mibuyu. Na hilo liangalie wazi kabisa, kwenye kila matatizo makubwa yanayotokea, wapo watu ambao hawaanguki, wanaendelea kuwepo na wanaendelea kukua.

Sasa kwa nini na wewe usiwe mmoja wa hao? Kwa nini na wewe usijijenge na kuwa imara kiasi kwamba pamoja na mengi yanayoweza kutokea ukaendelea kuwa imara?

Hili linawezekana, pale unapoamua kwamba hakuna kitakachokurudisha nyuma. Unachagua kile unachotaka kufanya kwenye maisha yako, na unapambana kukifanya, bila ya kukubali kikwazo chochote kikurudishe nyuma.

Unajitoa kuhakikisha unafika kule unakotaka kufika, unakuwa mbishi, unatafuta kila njia ya kutoka pale unapokwama. Na kwa njia hii, utakuwa mbuyu, mbuyu unaoogopwa na kila aina ya upepo.

Wewe mwenyewe umekuwa unajiangusha, pale unapokubali kirahisi unapokutana na vikwazo. Pale unapoanza kujitilia shaka wewe mwenyewe, na kujiuliza nitaweza kweli? Halafu wanatokea watu wanakuambia huwezi, achana na hiyo, na wewe unasema wapo sahihi, siwezi, naacha.

Pale unapokuwa na hofu kwamba utashindwa au utapoteza, pale unapokuwa na wasiwasi kwamba huenda usifike pale unapotaka kufika, unaruhusu upepo wa nje ukuondoe kabisa. Na ukweli ni kwamba, upepo ni mkali mno.

Kuwa imara au utapotezwa na kila aina ya upepo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.