Tamaa ni asili ya binadamu, kwa sababu mara nyingi huwa kuna msingi wa tamaa, ambao umetuzunguka, hivyo tunaposhindwa kuujua na kuufanyia kazi, tunaishia kuwa watu wa tamaa na kuumia sisi wenyewe na kuwaumiza wengine pia.
Msingi mkuu wa tamaa ni ujinga. Ni ujinga kwa sababu kinachomsukuma mtu kutamani vitu zaidi ni kitu ambacho siyo sahihi.
Kwa mfano, watu huwa na tamaa ya vitu fulani, wakiamini kwamba wakishapata vitu hivyo basi watakuwa na furaha sana kwenye maisha yao. Lakini ni mpaka pale wanapopata vitu hivyo, ndiyo wanagundua walikuwa wanakimbia kwenye njia ambayo siyo sahihi.
Watu huwa na tamaa ya vitu fulani, wakiamini kwamba wakipata vitu hivyo basi wanakuwa salama na maisha hayatakuwa na changamoto tena. Ni mpaka pale wanapopata vitu hivyo, ndiyo wanagundua wameingia kwenye changamoto kubwa kuliko walizokuwa nazo awali.
Tamaa ni ujinga kwa sababu hakuna chochote kinachoweza kushibisha tamaa. Kwa lolote lile, tamaa huwa inazidi kuwa kubwa kadiri mtu anavyokazana kuitimiza.
Hii ndiyo sababu wezi na mafisadi huwa hawafiki mahali na kusema basi imetosha, kwa sababu kadiri wanavyopata zaidi, ndivyo tamaa yao inazidi kuwa kali zaidi.
Hakikisha unadhibiti tamaa ya kila aina kwenye maisha yako, dhibiti kwa kuhakikisha unapata kile unachostahili na kwa njia sahihi, ambazo zinakubalika. Wakati wowote utakaposhawishika kupata usichostahili, na kwa njia ambayo siyo sahihi, unapanda mbegu ambayo itaendelea kukusakama maisha yako yote.
Usikubali ujinga wa kufikiri ukipata kitu fulani basi utakuwa na furaha, au utakuwa na usalama wa kutosha. Tamaa ikishakuingia kwa njia hii, unakuwa mtumwa wa vitu ambavyo ni vigumu mno kupata uhuru wake.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog