UKURASA WA 977; Tawala Hasira Zako…

By | September 3, 2017

Kitu cha kwanza muhimu kabisa unachopaswa kufanya kwenye maisha yako, ni kutawala hasira zako. Kuhakikisha hasira zako zinakuwa mbali sana kiasi kwamba haziwezi kufikiwa kirahisi.

Tawala hasira zako kiasi kwamba chochote kinachoweza kutokea, kinachosemwa au kufanyika unaendelea kubaki na utulivu wako.

Hili ni muhimu kwa sababu;

Wapo watu ambao watajaribu kukuudhi kwenye kila aina ya jambo.

Wapo ambao wanataka ukasirike, ufanye maamuzi mabovu halafu wao wanufaike.

Wapo ambao wanataka ukasirike, uhamishe nguvu zako kwenye kile unachofanya na usumbuliwe na kelele nyingine.

Unapokasirika, unazuia akili yako kufikiri kwa umakini na maamuzi mengi unayochukua yanakuwa siyo mazuri.

Mtu yeyote ambaye hawezi kutawala hasira zake, hawezi kufanikiwa, na chochote atakachojenga, atakuja kukibomoa.

SOMA; UKURASA WA 630; Hatua Za Kuchukua Kama Huwezi Kudhibiti Hasira Zako…

Tawala fikra zako, mara zote kuangalia upande mzuri na chanya kwenye jambo lolote, kwa sababu hasira zinapoingia zinazuia uwezo wako wa kufikiri sawasawa.

Tawala ulimi wako na kaa kimya pale ambapo unakasirishwa, kwa sababu hasira hutumia ulimi kutoa maneno ambayo siyo mazuri.

Tawala mwili wako kwa kujituliza pale unapokasirishwa kwa sababu mwili hujiandaa kwa mapambano unapokuwa kwenye hasira.

IMG-20170526-WA0000

Kadiri unavyoweza kutawala akili, mwili na roho, ndiyo hasira zako zinavyozidi kwenda mbali na kuwa mtulivu hata kama jambo kubwa na baya kiasi gani limetokea.

Na muhimu kabisa ni kukumbuka ya kwamba lolote linalotokea, kama bado upo hai basi maisha bado yanaendelea. Kosa lolote lililofanyika linaweza kurekebishwa au kuchukuliwa kwa jinsi lilivyo, muhimu ni maisha yasonge mbele.

Muhimu kabisa, jitawale wewe mwenyewe, hili litakuwezesha wewe kuwa na maisha ambayo unayataka wewe na siyo yale ya kusukumwa na wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.