UKURASA WA 978; Mambo Mawili Muhimu Kuhusu Fursa.

By | September 4, 2017

Kwanza; fursa ni nyingi mno, na zitaendelea kuwa nyingi kila siku.

Mbili; hakuna fursa ambayo ikikupita ndiyo basi tena, kwa kifupi huwezi kupitwa na fursa yoyote.

Nimeanza na hayo mawili kwa sababu wengi hawayaelewi au hawayakubali na hilo limekuwa linawaingiza kwenye matatizo makubwa.

Watu wengi wamekuwa wakiaminishwa kwamba kuna uhaba wa fursa. Kama vile kuna kiwango fulani cha fursa ambacho kinaisha. Hali hii imekuwa inawasukuma watu kukimbilia kuchukua fursa ambazo hawazihitaji, kwa kuamini kwamba hakuna zile fursa wanazotaka wao.

IMG-20170726-WA0003

Wengi pia wamekuwa wakiaminishwa kwamba fursa ikishakupita basi ndiyo umeshindwa kufanikiwa. Hilo limekuwa linawasukuma watu kuchukua hatua kabla hata hawajafanya utafiti wa kutosha kwa kuamini wakichelewa fursa hizo zitawapita.

Naomba nikuambie kwamba, yeyote anayekuambia kinyume na nilivyokuambia hapa, anakudanganya au kuna kitu anataka kukuuzia.

Ukiona mtu anakung’ang’aniza kwamba chukua hatua sasa la sivyo utakosa fursa hii, ni vyema ukajipa muda wa kusubiri na kuelewa kwanza, kama bado hujaelewa vizuri. Usikimbilie kufanya maamuzi kwa kuona unapoteza, utapoteza zaidi kwa kuchukua maamuzi ambayo huyaelewi, kuliko kutokuchukua hatua kabisa.

SOMA; Jinsi Ya Kuchagua Uwekezaji Unaokufaa Wewe Kulingana Na Mahitaji Yako.

Fursa zipo nyingi mno, nyingi kiasi kwamba huwezi kuzimaliza zote. Kila kitu ni fursa, kila kitu. Hivyo unachohitaji kufanya ni kuchagua fursa zipi unaziangalia wewe na kuzielewa kwa undani ili kuweza kuchukua hatua.

Pia fursa moja ikipita, nyingine zipo njiani zinakuja. Hivyo usidanganyike kwamba unachelewa, labda kama umeshapata taarifa zote muhimu, na unahitaji fursa hiyo, lakini ukachagua kusubiri, hapo umepoteza. Lakini kama kitu hujakielewa, halafu ukakimbilia kuchukua hatua ili usikose, unakuwa umechagua kukosa zaidi.

Nakukumbusha haya rafiki ili uwe makini, dunia ya sasa watu wanakuwinda sana, wapo wanaotaka kukuuzia vitu, wapo wanaotaka kukuibia na kukutapeli. Bila ya maarifa sahihi, utaona unachukua hatua sahihi lakini unashindwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.