UKURASA WA 981; Wewe Ni Bora Zaidi Ya Unavyofikiri…

By | September 7, 2017

Upo mtego mmoja mbaya sana kwenye maisha ambao wengi wameingia. Mtego huu kwa Kiingereza unaitwa learned helplessness, ambapo mtu anakuwa amepitia kushindwa mara nyingi na kujifunza kwamba yeye ni mtu wa kushindwa tu.

Hali hii inaanzia kwenye fikra na mazoea ambayo watu wanakuwa wamejengewa tangu wakiwa watoto. Wanayapokea kama sehemu ya maisha yao na hivyo kushindwa kupiga hatua.

learnedhelplessness

Kwa mfano mtu ambaye tangu akiwa mtoto amekuwa akiambiwa kwamba yeye ni mjinga, hana akili na hawezi kufanya lolote kubwa, atajifunza hivi na maisha yake yote atayajenga kwenye hali hiyo.

Kadhalika ambaye amekulia kwenye umasikini na kuambiwa yeye ni masikini na hakuna analoweza kufanya, anajifunza hilo na kukua nalo.

Hapo ulipo sasa, yapo mengi ambayo yanakuzuia kufanikiwa, ambayo umejifunza na siyo uhalisia. Kila kitu ambacho ukifikiria mafanikio kinajitokeza kwenye akili yako, ni ukomo uliojifunza, ambao unakuzuia.

SOMA; UKURASA WA 546; Kitu Kimoja Unachoweza Kukitegemea Hatakama Unakosa Vitu Vingi…

Ili kujua nini kinakuzuia, jiulize unawezaje kuwa na mafanikio makubwa sana kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako?

Ukianza kuona vitu vinakuja kwa njia ya, lakini huna hichi… jua hivyo ndiyo vikwazo ulivyojifunza.

Labda unapata wazo lakini sina elimu kubwa, basi jua umejifunza kwamba huwezi kufanikiwa kwa sababu huna elimu kubwa, kitu ambacho ni uongo.

Au likakujia wazo kwamba, lakini nimetoka kwenye familia masikini, hicho ndiyo kikwazo umejifunza na kinakuzuia kupiga hatua.

Chochote kinachokujua, iwe ni utegemezi mkubwa, kipato kidogo, kutokuthaminiwa, ni uongo ambao umeurudia kila siku kwenye maisha yako na sasa umeanza kuuamini kama ukweli.

Leo ninachotaka kukuambia ni hichi rafiki, wewe ni bora zaidi ya unavyofikiri. Unao uwezo mkubwa wa kufanya zaidi ya unavyofanya sasa. Hujui hili kwa sababu hujawahi kujaribu, mara zote umekuwa unafanya yale uliyozoea, ambayo yanaendana na zile hadithi umekuwa unajipigia kila siku.

Ni wakati sasa wa kutengeneza hadithi mpya ya mafanikio. Kila unapofikiria mafanikio, jipe sababu kwa nini utayafikia, na fikiria hizo kila unapoyaangalia mafanikio yako.

Badala ya kujiambia kwa nini utashindwa, jiambie kwa nini utaweza au kwa nini inabidi uweze. Hali hii itakusukuma na kukupa hamasa ya kuweka juhudi kuliko ile ya kuona huwezi au hustahili.

Jitengenezee hadithi kama wewe ni wa kipekee, hakuna kama wewe dunia nzima, hivyo haiwezekani kabisa ukawa umekuja hapa duniani kupita tu kimya kimya.

Jijengee hadithi inayojumuisha vipaji ulivyonavyo na uwezo mwingine wa kipekee uliopo ndani yako. Jipe mifano ya mambo umewahi kuyafanikisha, hata kama ni madogo kiasi gani, hayo yatakupa hamasa ya kuendelea zaidi.

Upo hapo ulipo kutokana na hadithi ambazo umekuwa unajiambia kila siku. Kama unataka kufika eneo tofauti na ulipo, hebu anza na hadithi tofauti na unazojiambia sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 981; Wewe Ni Bora Zaidi Ya Unavyofikiri…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.