Lipo neno kwa Kiingereza linaitwa ‘trade off’, ambapo hii ni dhana iliyo wazo kabisa kwamba kuchagua kufanya jambo moja, maana yake umechagua kutokufanya jambo jingine.
Na hili ni dhahiri kabisa kwenye muda, kwa sababu muda una ukomo usioweza kuongezwa na yeyote. Masaa 24 kwa siku ndiyo ambayo tunayo, hakuna wa kuongeza hata dakika moja.
Hii ina maana kwamba, kwa muda huu mfupi tulionao, unavyochagua kuutumia kuna madhara makubwa sana kwako. Kila ambacho unaruhusu kukifanya, maana yako unajizuia usifanye mambo mengine.
Hivyo basi, muda wowote ambao unautumia tofauti na kule ambapo unataka kwenda, ni muda ambao umechagua kuupoteza.
Muda ambao unaweza kuutumia kuanza kufuatilia maisha ya wengine, ni muda ambao ungeweza kuutumia kujifunza na kuwa bora zaidi.
Muda ambao unachagua kuperuzi mitandao ni muda ambao ungeweza kuuweka kwenye kazi zako na kuzalisha matokeo bora zaidi.
Muda ambao unautumia kufuatilia kila aina ya habari, ni muda ambao ungeweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; DEEP WORK (Mbinu Za Kufanya Kazi Yenye Maana Kwenye Zama Hizi Za Usumbufu).
Tatizo kubwa huwa tunaangalia muda tunaoutumia kwa wakati husika, na kuona ni muda mdogo.
Lakini tukianza kuangalia muda kwa thamani tunayoipoteza, hakuna muda mdogo kabisa. Kwa sababu hata dakika kumi unazoweza kutumia kuperuzi mitandao ya kijamii, ni dakika ambazo ungeweza kusoma angalau kurasa 5 mpaka 10 za kitabu. Sasa ukifanya hivyo kila siku, ndani ya mwezi mmoja unakuwa umemaliza kitabu. Je hapo utabaki kulalamika husomi vitabu kwa sababu huna muda?
Kila unapofikiria kuhusu muda, unapopata changamoto ya kuona muda hautoshi, anza kwanza kwa kuangalia kwa sasa kila dakika yako inaenda wapi. Usituambie huna muda au muda ni changamoto kwako, wakati kuna dakika nyingi ambazo unazitumia kwenye mambo yasiyo na mchango wowote kwenye mafanikio yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog