UKURASA WA 984; Usinunue Hofu Za Wengine…

By | September 10, 2017

Watu wenye hofu wana tabia moja, hawapendi kuwa peke yao.

Mtu anapokuwa na hofu, akiwa nayo peke yako inamtisha na kujiona labda ana matatizo makubwa.

Ili kuepuka hilo, huwa wanatafuta watu wengine ambao nao watakuwa na hofu kama ambayo wao wanayo.

Na hapo ndipo wanapoanza kusambaza hofu hiyo kwa wengine. Wanatumia kitu ambacho ni halisi, kuzalisha hali ambayo siyo halisi.

IMG-20170726-WA0003

Kama lipo tatizo dogo basi wanalikuza mpaka linaonekana ni kubwa na litazidi kuwa kubwa sana.

Kwa njia hii wanasambaza hofu, watu wanakuwa kwenye hali ya wasiwasi na hiyo inakuwa furaha yao kwa sababu sasa wengi wana hofu kama yake.

Usisahau kwamba watu wanapokuwa kwenye kundi la watu wengi huwa wanajisikia salama, hata kama kundi hilo halipo sahihi.

SOMA; UKURASA WA 887; Giza Haliwezi Kupona Hapa…

Hivyo basi rafiki yangu, unahitaji kuwa makini sana na watu wanaokuzunguka au wanaoweza kukupa taarifa yoyote. Mara nyingi wale wanaokupa taarifa mbalimbali, huwa wanazitengeneza kwa njia ambayo zitakujengea hofu kama ambayo wao wanayo.

Njia bora ya kuepuka hili ni kuchukulia kila taarifa unayopewa na wengine yenye hofu kama taarifa kiasi, ambayo hujapata ukweli kamili, na hivyo usizame moja kwa moja kwenye hofu. Tafuta ukweli kamili ili ujue hatua za kuchukua.

Watu wakishaanza kugundua kwamba hata ukipewa taarifa za hofu huingii kwenye hofu mara moja, watakuwa wanaachana na wewe. Watakuwa wanatafutana wao kwa wao na kujazana hofu, wewe utakuwa siyo mteja mzuri wa hofu zao.

Usiambiwe kitu na wewe ukachukulia kama ndiyo ukweli wenyewe. Badala yake dadisi, hoji, chunguza, ukianza na wale wale ambao wanakupa taarifa za hofu.

Mambo muhimu ya kukumbuka;

Hofu haijawahi kubadili chochote.

Hofu ni hali ya kutengenezwa na mtu kulingana na taarifa anazopokea.

Hofu haikuwezeshi kuchukua hatua yoyote.

Wakati wowote unapokuwa kwenye wasiwasi, fanya kitu sahihi, mara zote itakuletea matokeo sahihi. Lakini kuhofia, kunakufanya ushindwe kuchukua hatua sahihi.

Usinunue hofu za wengine, usiwauzie wengine hofu zako, ukiwa na wasiwasi, fanya kitu sahihi, kitu chenye msaada kwa wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 984; Usinunue Hofu Za Wengine…

  1. Pingback: UKURASA WA 1100; Mtu Pekee Wa Kumwonea Aibu Ni Huyu… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.