UKURASA WA 988; Kabla Hujazama, Elewa Misingi…

By | September 14, 2017

Hakuna watu hatari kama waliozama na kubobea kwenye jambo lolote kabla hawajaielewa misingi. Kwa sababu uzamivu wao, hugeuka kuwa hatari kwao na kwa wengine kuliko unavyokuwa faida, hata kama ni kwa jambo zuri.

Chukua mfano wa fedha, kila mtu anapenda fedha, kila mtu anakazana kupata fedha, lakini mtu anapozama kutafuta fedha kabla ya kuijua misingi ya fedha, mambo huwa mabaya mno.

Hapa ndipo watu hujikuta wakifanya mambo yasiyo sahihi kwa sababu wanaona tu watapata fedha, kwa mfano kucheza kamari na michezo ya kubahatisha.

Wakati mwingine watu hutumia njia zisizo sahihi, ulaghai na utapeli ili tu wapate fedha.

IMG-20170726-WA0003

Hapo bado hujaingia kwenye madeni, ambapo watu wanakazana kukopa wakiamini mikopo ni ukombozi kwao kumbe ndiyo shimo baya zaidi kwao kifedha.

Utaona watu wanakazana kufanya kila aina ya kitu, wao wanaona wapo kwenye njia sahihi lakini ukiangalia misingi, wapo nje ya misingi.

Katika jambo lolote lile, ukienda nje ya misingi, huwezi kubali salama. Misingi ndiyo kila kitu, misingi haivunjwi na misingi haina huruma kwa mtu yeyote yule. Ni uchague kuielewa na kuifuata mambo yaende vizuri kwako au ipuuze na kuivunja na mambo yaende vibaya kwako.

SOMA; UKURASA WA 636; Ishi Maneno Yako…

Kila jambo kwenye maisha, kila kitu tunachofanya, kina misingi yake. Kila kitu unachotaka kuwa bora, kina misingi yake. Na kama unataka maisha yako yawe bora na yenye mafanikio, unapaswa kujitengenezea misingi yako ambayo utaifuata kila wakati. Hiyo inakuwa ndiyo katiba yako, ambayo hutaivunja.

Kuna wakati misingi inaweza kuonekana migumu na isiyowezekana, lakini hayo yote yanatokana na hali ambayo jamii imejijengea hasa ya mtu kupata zaidi ya anavyostahili, au kupata zaidi ya alivyoweka.

Kama kwenye fedha, ukishataka kupata fedha nyingi zaidi ya juhudi unazoweka na thamani unayotoa, lazima uishie kwenye wizi, ulaghai, utapeli au kamari. Kwa sababu hizo ndizo njia pekee zinazoruhusu hali hiyo. Sasa unaweza kutumia njia hizo ukapata mara moja, lakini utarudisha au kupoteza kila ulichofanya. Ni msingi, hauvunjiki hata kama unaona uko sahihi kiasi gani.

Kabla hujazama na kubobea kwenye jambo lolote, ielewe kwanza misingi na kamwe usiivunje misingi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.