UKURASA WA 992; Mambo Yangeweza Kuwa Mabaya Zaidi…

By | September 18, 2017

Kila mmoja wetu kuna wakati anapitia changamoto na matatizo mbalimbali kwenye maisha yake.

Hali hizi huwa zinasikitisha na kukatisha tamaa. Wakati mwingine mtu unaona kama kuna giza mbele yako na hujui hatua gani tunaweza kuchukua kuondoka kwenye hali ile.

Lakini ukweli ni kwamba, hali yoyote ambayo tumekutana nayo, na changamoto yoyote ambayo tunapitia, mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi.

Kila Changamoto

Kama unapitia changamoto ya ugonjwa, jua mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi, labda ukawa na kilema au hata kufa kabisa. Hivyo kuwa na ugonjwa ambao unaweza kutibika na ukarudi kwenye afya yako, siyo jambo baya kama unavyofikiri.

Kama changamoto yako ni ajira ambayo huipendi na haikuridhishi, jua mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi. Inawezekana ungekuwa huna ajira kabisa, au una ajira yenye mateso zaidi ya uliyonayo sasa. Hivyo kuwa tu na ajira usiyoipenda au isiyokulipa, ni njia ya wewe kwenda kule unakotaka.

Inawezekana pia una ndugu au jamaa ambao ni wasumbufu, wanakupa changamoto na hawashukuru kwa lolote unalofanya. Lakini angalau unao watu hao, ambao unaweza kusema ni ndugu na jamaa, angalau haupo peke yako porini, ukikazana kulinda maisha yako. Mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi.

SOMA; Uongo Huu Unaojiambia Kila Siku, Ni Adui Mkubwa Wa Mafanikio Yako.

Kwenye kila hali tunayopitia, hata kama ni ngumu kiasi gani, kumbuka mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi. Hata kama umepata ajali mbaya sana, angalau upo hai, wengi wanapata ajali na kupoteza maisha yao.

Hii inatukumbusha umuhimu wa kushukuru kwa kila jambo, kuacha kuangalia upande wa ubaya wa jambo na kuona ni hatua zipi tunazoweza kuchukua ili kufanya jambo lolote kuwa bora zaidi na maisha yetu kuwa bora pia.

Kama bado upo hai, basi hali yako bado siyo mbaya kama unavyofikiri, na kazi yako hapa duniani bado haijaisha. Hivyo haijalishi umeanguka mara ngapi, haijalishi umekutana na vikwazo vya aina gani, amka na endelea na mapambano.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.