Unaweza kupiga hatua moja kwa wakati, na ukaendelea hivyo mpaka ukafika mbali mno. Hata kama umechelewa kiasi gani, ukikazana kupiga hatua mbili kwa wakati mmoja, hutaenda mbele, badala yake utaanguka.
Wahenga pia walishatuambia anayekimbiza sungura wawili, hawezi kumkamata hata mmoja. Kwa sababu wote wanakupa tamaa na mwisho kila mmoja atakimbilia upande wake. Ni bora kuchagua sungura mmoja na ukaweka nguvu zako zote kumkimbiza mpaka umpate.
Sasa tunasahau misingi hii inapokuja kwenye akili zetu wenyewe. Tumekuwa tunazitumia akili zetu kwa makosa na hivyo kushindwa kuzifaidi vizuri.
Akili zetu zinaweza kufanya jambo moja kazi kwa wakati, kwa ufanisi wa hali ya juu. Lakini mambo yanapokuwa mengi kwa wakati mmoja, ufanisi unapungua na tunaanza kupata matokeo mabovu.
Unapokuwa na jambo moja, wazo moja ambalo lipo kwenye akili yako kwa wakati, na kuitaka akili yako ilifanyie kazi, akili itakuletea kila fursa ya wewe kuweza kulifanyia hilo kazi.
SOMA; UKURASA WA 804; Kama Kila Kitu Ni Kipaumbele, Huna Kipaumbele….
Lakini unapokuwa na mambo mengi kwenye akili yako, mawazo yako yanahama hama kwenye mambo hayo, na unapoteza nguvu nyingi kwenye kuhama hama kwa mambo, ambayo ungeweza kuitumia kwenye kuongeza ufanisi.
Ili kuhakikisha akili zetu zinatupa matokeo bora kabisa, na kutuwezesha kuziona fursa tunazohitaji ili kupiga hatua, tunahitaji kuwa na jambo moja kwa wakati kwenye akili zetu. Turuhusu wazo la kitu kimoja pekee kutawala akili zetu.
Kwa maana hii, tunahitaji kufanya jambo moja kwa wakati, na tunahitaji kuyadhibiti mawazo yetu kuwa kwenye jambo lile tunalofanya. Tusiruhusu mawazo yetu yazurure huku na huko, tutapunguza ufanisi wetu.
Weka mawazo yako kwenye kile unachofanya, kwa wakati ambapo unakifanya, ukishamaliza unaweza kuyapeleka kwingine unakotaka.
Kufanyia kazi vitu vingi kwa wakati mmoja, kunaijaza akili na mambo yasiyo muhimu, kunazuia uwezo wetu wa kuona fursa zaidi kwenye kile tunachofanya na kupunguza ufanisi wa akili zetu.
Kufanya jambo moja kwa wakati, na kudhibiti akili ifikirie kile tunachofanya pekee, ni njia ya uhakika ya kupata matokeo mazuri ndani ya muda mfupi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog