UKURASA WA 998; Kushinda Kwa Gharama Yoyote Ile…

By | September 24, 2017

Kila mmoja wetu anapenda ushindi,

Kila mmoja wetu anapanga kushinda,

Na baadhi yetu tunachukua hatua katika kuelekea ushindi.

Tunapochukua hatua, tunagundua jambo moja kubwa, ushindi una gharama, na gharama yake inaweza kuwa kubwa sana.

Wale ambao wapo tayari kulipa gharama, ndiyo wanaoshinda. Lakini wasiotaka kulipa gharama, hawana nafasi ya ushindi kwenye haya maisha.

Njia Panda

Lakini kwenye kulipa gharama nako pia kuna changamoto kubwa.

Ipo gharama ya kawaida ya kulipa, ninaposema ya kawaida simaanishi ni ndogo, bali ni gharama ambayo haina madhara makubwa kwako ukilinganisha na ushindi unaopata.

Lakini pia ipo gharama ambayo siyo ya kawaida kulipa, hii ni gharama ambayo ni kubwa ukilinganisha na ushindi unaopata. Yaani unalipa gharama, unapata ushindi, lakini unajutia kile ulichofanya.

Hii ndiyo gharama mbaya sana ambayo wachache wameingia. Wale ambao wanasema wapo tayari kushinda kwa gharama ya aina yoyote ile, huwa wanaingia kwenye mitego ambayo inakuwa kifungo kikubwa cha maisha yao, licha ya kuwa washindi.

Kwa mfano mtu ambaye yupo tayari kulipa gharama kubwa ya muda wa kufanya kazi na biashara zake. Ambaye muda wote ni kazi, hana muda hata mdogo wa kupumzika, hapati muda wa kula kwa afya na hapati muda wa kuwa karibu na familia. Anapambana na kufanikiwa, lakini afya yake inakuwa mbovu, mahusiano na familia mabovu. Ule ushindi wake unakuwa hauna maana tena.

Au mtu ambaye anasema yupo tayari kufanya lolote ili tu apate fedha. Anajihusisha kwenye biashara au mambo ambayo siyo halali, labda anatapeli wengine, au anajihusisha na ufisadi, anapata fedha kweli, lakini hawezi kuzifurahia. Hawezi kukaa mahali akafurahia fedha hizo kwa kuishi maisha anayoyataka. Badala yake muda wote anajificha, au anakuwa na kesi zinazomaliza muda wake.

SOMA; UKURASA WA 375; Fikra Potofu Kuhusu Mafanikio…

Ninachokuambia rafiki ni siyo usilipe gharama, bali angalia gharama unayolipa, baadaye itakuweka kwenye hali gani? Usiangalie tu kile unachopata leo, bali angalia maisha miaka 10, 20 na hata 50 ijayo. Kwa kuendelea kufanya unachofanya sasa, je utakuwa katika hali gani?

Zipo gharama nyingi ambazo unaweza kulipa bila hata ya kujiuliza, mfano kuacha kuangalia tv, kusoma magazeti, kutembelea mitandao ya kijamii, kununua vitu vya anasa, kutumia vilevi, kushiriki kwenye majungu na umbeya. Hivi na vingine vinavyofanana navyo, unaweza kuachana navyo na maisha yako yakawa bora zaidi.

Lakini zipo gharama ambazo usijaribu kabisa kulipa, mfano kukosa muda wa kutunza afya yako, kukosa muda na familia na watu wa karibu kwako, kufanya jambo ambalo siyo sahihi. Hizi usiguse kabisa, kwa sababu malipo yake ni makubwa kuliko utakachokwenda kupata.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.