UKURASA WA 1003; Njia Bora Ya Kuwakasirisha Wanaokukasirisha…

By | September 29, 2017

Changamoto kubwa za maisha yetu zinaanzia kwa wale wanaotuzunguka. Msongo wa mawazo, hasira, chuki, wivu na hisia nyingine za aina hiyo, zinatoka kwa wale wanaotuzunguka. Kadhalika pia hisia nzuri za furaha, matumaini, upendo tunazipata kutoka kwa wengine.

Wapo watu ambao wanafanya mambo fulani kwa makusudi, ili wewe ukasirikie. Wengine wanafanya hivyo kwa sababu tu wanaona wewe umepiga hatua na kuwaacha. Wengine wanafanya hivyo kwa sababu wanajua ukikasirika utachukua hatua ambazo siyo nzuri na wao watanufaika na hatua hizo unazochukua.

Sasa hatua bora ya kuchukua kwa wale wanaokukasirisha au kukuudhi siyo wewe kukasirika au kuudhika. Badala yake unahitaji kuchukua hatua ya kuwakasirisha zaidi. Na hufanyi hivyo kwa kuchukua hatua za kuwakasirisha kama wao wanavyofanya. Bali unachofanya ni kutojibu yale wanayofanya ya kukukasirisha.

Unachofanya ni kuwa mtulivu, kutokustushwa na yale ambayo watu wanafanya ili ukasirike. Pale mtu anapotoa maneno makali na machafu, anapojipandisha hasira ili na wewe upate hasira, wewe unatulia kama vile hakuna kitu kinachoendelea. Unakuwa mtulivu, unakuwa na subira.

Hakuna kitu kinamkasirisha mtu kama hicho, kadiri unavyokuwa mtulivu na mwenye subira, yule anayetaka kukupandisha hasira anakasirika yeye zaidi. Anashindwa kabisa kukuelewa inakuwaje pamoja na hayo yote umetulia. Hili linajenga hofu kubwa kwake, anashindwa kukuelewa na anakosa sababu ya kuendelea.

SOMA; MATUSI ; Jinsi ya kukabiliana na dharau za wengine.

Hakuna nguvu kubwa kama hii, ambayo tayari unayo ndani yako, ya kukuwezesha kuvuka changamoto unazowekewa na wengine. Watu wengine wanaweza kuwa na hofu, ila hawawezi kuvumilia hofu zile wao wenyewe, hivyo wanazisambaza, kwa kuzijaza chumvi ili na wengine nao wahofie. Sasa ukiwa mtu mtulivu, mwenye subira, watu hawatajisumbua kukuletea hofu zao.

Hili pia linafanya kazi sana kwenye watu wanaojenga chuki dhidi yako. Chuki ya mtu kwako, haitakamilika mpaka na wewe ujibu chuki ile. Sasa usipojibu ile chuki, yaani mtu akikuchukia lakini wewe ukampenda, au usioneshe tofauti yoyote, atajidharau yeye mwenyewe.

Utulivu na uvumilivu vitakusaidia sana, tena sana kwenye kila wakati mgumu unaoweza kuwa unapitia kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

2 thoughts on “UKURASA WA 1003; Njia Bora Ya Kuwakasirisha Wanaokukasirisha…

  1. mohd

    Umesema ukweli Coacher. Njia ya kushinda majaribu ya kukasirishwa na wengine ni kuwa mtulivu na kuendelea Kuwaza na kupanga mikakati ya maendeleo uliyonayo mtu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.