Tunapoanza kufanya kitu chochote, iwe ni kazi, biashara na hata maisha ya kawaida, huwa kuna viwango ambavyo tunajiwekea. Huwa tuna picha ya namna tutakavyokuwa tunafanya, huwa tuna malengo na mipango mikubwa ya kile tunachofanya.
Lakini tunapoanza kufanya, tunakutana na dunia, tunakutana na wale ambao wanafanya kile tunachofanya. Na tunagundua, wengi hawafanyi kama sisi tulivyokuwa tunafikiria kufanya. Wengi wanafanya kwa viwango vya chini kuliko tulivyokuwa tunafikiria sisi.
Na kwa kuwa ni wengi wanafanya vile, tunaanza kuona huenda wengi hao wapo sahihi. Na ndiyo kimewafanya wakaweza kufanya. Hapo inatubidi kushusha viwango vyetu, na kufanya kama wanavyofanya wengine.
Hapo ndipo wengi wanazifukia ndoto zao, hapo ndipo wengi wanaamua kuondoka kwenye njia ya mafanikio, na kuishia kuwa kwenye kundi la wengi, ambao wanafanya kawaida na hawaendi popote.
Wakati mwingine watu wanaanza kufanya, kwa kuzingatia viwango walivyojiwekea, lakini wanakutana na vikwazo na changamoto, na hapo wanachagua kushusha viwango walivyojiwekea, kwa kuona kufanya hivyo kutapunguza changamoto.
Hivyo unapoanza kufanya jambo lolote, usikubali kabisa kushusha viwango vyako, iwe ni kwa sababu umeona wengine wanavyofanya au iwe umekutana na changamoto. Unaweza kushusha viwango vyako na ukafanya kama wengine wanavyofanya, lakini kumbuka hutakuwa unatumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako.
Na kama umeshusha viwango ili kukimbia changamoto, jua changamoto zile hazitaondoka, hivyo uchague kuendelea na viwango hivyo vya chini au uchague kutatua changamoto hiyo na kusonga mbele.
SOMA; UKURASA WA 640; Hichi Ndiyo Unapata Kwenye Maisha Yako…
Wewe pekee ndiye unayejijua zaidi ya wengine wanavyokujua, wewe ndiye unayejua ndoto zako kubwa, wewe ndiye unayejua unataka nini. Usikubali ushawishi wa mtu yeyote ukuondoe kwenye njia yako ya mafanikio.
Weka viwango vikubwa na vifanyie kazi, hata kama hutavifikia, lakini utakuwa tofauti kabisa na wengine wote wanaofanya kile unachofanya wewe. na utofauti ndiyo unatengeneza mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog