Huwa tunaweka mipango mikubwa na mizuri sana ya maisha yetu. Tunapanga nini tunafanya na tunachukua hatua ya kufanya.
Lakini tunapoanza kufanya, tunakutana na kitu ambacho hatukutegemea, ugumu, vikwazo na changamoto.
Hali hizo tunazokutana nazo, zinatusababishia maumivu ambayo yanaweza kuwa ya mwili au akili, safari inakuwa ngumu kwetu kuliko tulivyotegemea.
Ni katika nyakati kama hizo ambapo akili inatupeleka kwenye majaribu, akili kwa kuwa haipendi maumivu, inaanza kutushawishi tuache.
Hapa ndipo tunapoanza kufikiria kwamba tulichokuwa tunafanya siyo muhimu kama tulivyofikiri, au tunajiambia kwa sasa tumekosea, tutafanya vizuri zaidi baadaye. Akili inaweza kutudanganya kabisa kwamba tulichofanya kinatosha, tunaweza kuishia hapo.
Kama usipokuwa makini na akili yako, itakuwa vigumu sana kujua kama kweli umefika mahali pazuri au akili inakudanganya na kukimbia maumivu.
Tunapaswa kuwa makini na kuona mawazo ya kuacha au kukata tamaa yamekuja wakati gani. Kama yamekuja baada ya kukutana na vikwazo, changamoto na maumivu, basi jua akili yako inakudanganya. Na chochote unachojiambia wakati huo siyo ukweli, ila tu unatafuta njia ya kukimbia.
SOMA; UKURASA WA 171; Unapokata Tamaa Maana Yake Umekubali Hivi.
Hadithi ya sizitaki mbichi hizi ina uhalisia mkubwa sana kwenye maisha yetu. Tunakitamani kitu na kuona tunaweza kukipata. Tunaweka juhudi kukipata lakini juhudi hizo zinakwama. Tunajiambia kwamba wala hatukukitaka sana, au siyo kizuri kama tulivyofikiri.
Unapochagua kufanya kitu, hakikisha unakwenda nacho mpaka mwisho, unapokutana na vikwazo na changamoto, usiisikilize akili yako pale inapokupa sababu kwa nini uache. Endelea kama ulivyopanga, akili itatulia na utaweza kupiga hatua nzuri, licha ya vikwazo na changamoto unazoweza kuwa umekutana nazo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog