UKURASA WA 1009; Matokeo Ni Muhimu Zaidi Kuliko Maelezo…

By | October 5, 2017

Kama unataka kuwashawishi watu kufanya kitu, kuchukua hatua fulani ambayo unaamini ni muhimu na bora kabisa kwao, unaweza kutumia njia mbili.

Njia ya kwanza ni kuwaeleza kwa kuwaambia kipi wanapaswa kufanya. Kuwaeleza kwa kina kila hatua wanayopaswa kuchukua. Na ili kuhakikisha wanahamasika hasa kuchukua hatua, itakuhitaji kukamata hisia zao pia.

Hivyo utahitaji kuweka maneno yenye hofu au tamaa. Maneno hayo yanawapa hofu fulani iwapo hawatachukua hatua, au kuwapa tamaa ya kuchukua hatua ili wapate kitu fulani.

Njia hii ya kwanza ni njia rahisi kutumia, njia ambayo wengi wanaitumia, kwenye biashara, kazi, mahusiano na kila sehemu ya maisha.

Lakini ni njia ambayo kwa sasa inakuwa sugu, kwa sababu kila mtu anasema, kila mtu anaeleza, kila mtu anahamasisha na watu wanazoea na kuona hakuna jipya.

Njia ya pili ni kuonesha matokeo, kuwaonesha watu kile ambacho wewe umepata kwa kuchukua hatua ambazo unawataka wao wachukue. Kwa njia hii, watu wanajionea wenyewe, wanayaona matokeo, na matokeo hayo yanahamasisha kuliko maneno pekee.

Njia hii ni ngumu na inahitaji muda, siyo ya haraka haraka kama ya maneno na maelezo. Inahitaji mtu uamini kweli kwenye kile unachowataka wengine wafanye, kiasi cha kufanya wewe mwenyewe na kupata matokeo mazuri.

Njia hii pia inaweza isiwavutie wengi, kwa sababu wengine wakiona mchakato unaopelekea matokeo, wanaona ni mgumu na hawauwezi. Lakini njia hii itawaleta watu sahihi, wale watu ambao watachukua hatua na kupata matokeo mazuri.

SOMA; UKURASA WA 789; Kutenda Na Kuitikia Matendo Ya Wengine…

Maisha yetu ya kila siku tuna nyakati tunazohitaji watu wakubaliane na sisi, wafanye kile ambacho tunawataka wafanye. Hakikisha wewe unakuwa mtu wa kwanza kufanya, kisha wengine waige mfano kwako. Itakuwa vyema kwako kama wale unaotaka wafanye ni watu sahihi unaowalenga, na siyo tu kila mtu.

Kwenye biashara, hakikisha wewe ndiye mteja namba moja wa biashara yako, unakuwa wa kwanza kutumia kile unachowauzia wengine, na una mifano ya wazi na hadithi za matokeo uliyoyapata au unajua wengine wamepata kupitia biashara hiyo.

Tumeshahama kutoka kwenye ulimwengu wa kuwashawishi wengi, na sasa tupo kwenye ulimwengu wa kuwagusa wachache moja kwa moja na kutengeneza mahusiano mazuri, yanayopelekea kupata kile ambacho kila mtu anataka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.