Kwenye masoko ya mitaji tumekuwa tunajifunza amana za aina mbili, hisa na hatifungani.
Katika uwekezaji kwenye amana hizi, mwekezaji anaweza kuchagua yeye mwenyewe anunue hisa na hatifungani zipi. Lakini hili linamtaka awe mfuatiliaji wa karibu wa hisa na siko la hisa kwa ujumla.
Wakati mwingine kuchagua hisa zipi nzuri kununua inaweza kuwa changamoto kubwa kwa mwekezaji mmoja mmoja, hasa ambaye hana uelewa mkubwa wa soko la hisa.
Pia kusubiri wakati wa kununua na kuuza hisa inaweza kuwa changamoto kwa wawekezaji pia.
Changamoto hii inatatuliwa na mpango wa pamoja wa uwekezaji. Huu ni mpango ambapo wawekezaji wanakusanya mtaji wao pamoja kupitia taasisi ambayo ina wataalamu wa uwekezaji, kisha taasisi hiyo kuwekeza kwa niaba yao.
Mpango wa pamoja wa uwekezaji unampunguzia mwekezaji jukumu la kuanza kufuatilia hisa moja moja na kujua ipi kwake inafaa kununua. Taasisi zinazoendesha mipango hii ya uwekezaji huwa na wataalamu wa uwekezaji na mipango ya uwekezaji ambayo inafanya mtaji kuwa salama.
Mpango huu wa pamoja wa uwekezaji pia unarahisisha ununuaji na uuzaji wa uwekezaji kwa wawekezaji. Badala ya mwekezaji kwenda kujaza fomu ya kununua hisa kila mara anaponunua, akishajiunga na mpango wa pamoja wa uwekezaji mara moja, anachoendelea kufanya ni kutuma fedha kwenye akaunti yake, kama anavyoweka fedha zake benki.
Pia katika uuzaji wa uwekezaji ambao mtu amefanya, anajaza fomu kwenye taasisi ya mpango wa pamoja wa uwekezaji, kisha kuwekewa fedha kwenye akaunti yake.
Kwa hapa Tanzania, taasisi zinazoendesha mpango wa pamoja wa uwekezaji ni UTT AMIS kupitia mifuko yake ya UMOJA na mifuko mingine waliyonayo.
SOMA; FURSA; Uwekezaji Kupitia Vipande Vya UTT.
Kwa wawekezaji wadogo na wanaoanza, ni muhimu sana kuwekeza kupitia UTT kwa kuwa na akaunti ya mfuko wa umoja, ambapo kila mwezi unatuma kiasi fulani cha fedha ambacho kinawekezwa.
Uzuri wa uwekezaji huu kupitia UTT ni kwamba unaweza kuwekeza kiasi kidogo cha fedha, kuanzia shilingi elfu 10, pia unaweza kutuma kwa njia za huduma za kifedha za simu kama MPESA na TIGO PESA.
Kupata maelezo zaidi kuhusu uwekezaji kupitia UTT tembelea tovuti yao kwenye http://www.uttamis.co.tz/
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog