Mti wa mwembe, unafanya kazi moja muhimu, kutoa matunda ya maembe wakati wa msimu wa maembe. Mti huo utafanya hivyo kila wakati wa kutoa maembe, bila ya kujali nani anakula maembe yale, au aliyeyala alishukuru au la. Na hata kama hali ya hewa siyo nzuri, bado utatoa maembe ila kwa viwango tofauti. Huo ndiyo wajibu wa mti wa embe, na miti mingine, kufanya kile ambacho inapaswa kufanya, bila ya kuangalia mambo mengine yanaendaje.
Vipi sasa kama mafanikio yangekuwa wajibu wako?
Kwa sababu watu wengi wamekuwa wanachukua mafanikio kama chaguo, kitu ambacho labda wanaweza kukifikia, au kinaweza kutokea. Siyo kitu kikuu cha maisha yao na hivyo hawakifanyii kazi kwa uhakika.
Lakini unapoyafanya mafanikio kuwa wajibu wako, unakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuyafikia. Unachukua hatua za mafanikio kama sehemu ya maisha yako, hivyo hutachoka wala kuona kama maisha kwako ni mateso, bali utafanya kwa sababu ndiyo unachopaswa kufanya.
Mafanikio yakishakuwa wajibu kwako unakuwa na kusudi kubwa zaidi ya kutengeneza fedha pekee. Utakuwa tayari kutoa zaidi ya unavyotegemea na zaidi ya wengine wanavyotoa. Utakwenda hatua ya ziada kuhakikisha unatoa kile unachopaswa kutoa, na wala hutajali kama unapokea au la. Lakini utakapofanya, hakuna namna utaacha kupokea zaidi.
SOMA; Mambo Haya Manne Yanakuzuia Wewe Kufikia Ukuu Kwenye Maisha Yako. Yajue Na Uyaepuke Ili Kufanikiwa.
Tuachane na dunia ambayo inachukulia mafanikio kama kitu cha kujaribu, au kuchagua kama kinawafaa au la. Sisi tuchukue mafanikio kama wajibu wa maisha yetu, matokeo ambayo tunapaswa kuyazalisha kupitia kile tunachofanya, bila ya kujali wengine wanafanya nini au wanachukuliaje.
Mafanikio ni wajibu, ni kitu ambacho inabidi tufanye, ndiyo maisha yetu, hatuna namna ya kukwepa. Tukiweza kufikia hatua hii, hakuna yeyote au chochote kinachoweza kutuzuia kufanikiwa. Kwa sababu wa kwanza kabisa kutuzuia ni sisi wenyewe.
Chukua mafanikio yako, kama wajibu wako namba moja hapa duniani. Jichukulie wewe kama mti wa mwembe, ambao wajibu wake ni kuzalisha maembe. Wewe zalisha mafanikio kwenye kile unachofanya na maisha unayoishi, kwa sababu, ndiyo wajibu wako, ndiyo sababu ya wewe kuwa hai.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog