Kuna safari moja, kwenye njia moja ambayo kuna mtu mmoja pekee anayeweza kufanya safari hiyo. Mtu huyo ni wewe mwenyewe.
Wewe, upo mmoja tu hapa duniani, hakuna kama wewe, hajawahi kutokea na wala hatakuja kutokea. Na hii ndiyo siri kubwa sana ya maisha yetu hapa duniani, ambaye hakuna aliyeweza kuing’amua.
Yote hayo unayajua, kwa sababu nimekuwa nakueleza mara kwa mara. Na leo nakueleza tena kwa sababu watu wengi wamekuwa wanakubali kuwapa watu wengine majukumu ya kuwaamulia wafanye nini na wasifanye nini. Kipi wanaweza kufanya na kipi hawawezi.
Mimi ninachokutaka ni urudishe uhuru huo kwenye mikono yako, kwa sababu hakuna anayekujua wewe kuliko wewe mwenyewe. Na kwa bahati mbaya zaidi, wewe mwenyewe unaweza usijijue vizuri.
Hivyo basi, utofauti wako hapa duniani, unapaswa kuutumia vizuri ili kuacha alama hapa duniani na kufanya maisha yako kuwa na maana.
Kama kuna kitu kikubwa unataka kufanya, akajitokeza mtu na kukuambia huwezi kwa sababu wapo waliojaribu wakashindwa, hupaswi kukubaliana naye kirahisi. Kwa sababu ni wengine wamejaribu wakashindwa, siyo wewe. Kuna wewe ambaye hujafanya kabisa, jipe nafasi ya kufanya, jipe nafasi ya kujaribu na utajifunza mengi mno, iwe utafanikiwa au utashindwa.
SOMA; UKURASA WA 668; Vitu Vitatu Vinavyokutengeneza Wewe Kama Ulivyo.
Unapoanza kufanya kitu chochote kipya, anza kwa matumaini ya kuweza kufanya makubwa, anza na picha kubwa kwa maono makubwa. Fikiria kwamba kila kitu kinawezekana, na kwa upekee wako, pale wengine waliposhindwa wewe utaweza kupiga hatua zaidi. Fanya jambo sahihi mara zote, na utaweza kufanya kile ambacho ni cha kipekee kabisa kwako.
Usiruhusu maoni ya wengine yawe kikwazo kwako kuchukua hatua. Hakuna maoni yanayoujua ukweli wako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog