3010; Kumpika chura.
Rafiki yangu mpendwa,
Ukitaka kumpika chura aliye hai, usimweke kwenye maji ya moto.
Kwa jinsi mwili ww chura ulivyo, ukimweka kwenye maji ya moto, atatoka kwa haraka sana.
Maji hayo ya moto yatampa nguvu ya ajabu ya kuweza kutoka haraka.
Unachopaswa kufanya ili utimize lengo lako la kumpika chura aliye hai ni kumweka kwenye maji ya baridi, kisha kuanza kuyapasha maji hayo moto kidogo kidogo.
Kwenye maji ya baridi mwili wa chura unakosa nguvu, hivyo anatulia.
Unapoanza kuyapasha maji moto kidogo kidogo, chura anajisikia vizuri, hivyo hatoki kwenye maji hayo.
Kadiri maji yanavyoendelea kuwa ya moto ndivyo yanavyoathiri misuli ya chura na inapofika hatua maji yamekuwa ya moto sana na anataka kuruka, anashindwa kwa sababu misuli yake inakuwa haina tena nguvu.
Rafiki, kuna masomo mengi sana ya kujifunza kwenye mfano huu wa kumpika chura, lakini hapa tutajikita zaidi eneo la mabadiliko.
Unapotaka kuleta mabadiliko kwenye kitu ambacho kinahusisha watu wengine, kufanya mabadiliko makubwa na ya haraka kutazalisha upinzani wa hali ya juu sana.
Watu watapinga na kuyazuia mabadiliko hayo yasifanikiwe.
Lakini kama utaenda na mabadiliko hayo kidogo kidogo na hatua kwa hatua, upinzani hautakuwa mkubwa.
Na baadaye wakati mabadiliko yanakuwa makubwa, watu wanakuwa wameshazoea kiasi kwamba hawana tena nguvu ya kupinga.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwako binafsi, unapotaka kufanya mabadiliko, ukianza kwa wingi na ukubwa, mwili wako wenyewe utakuletea mapingamizi mengi. Unaweza hata ukaumwa, ili tu usiendelee na mabadiliko uliyodhamiria.
Lakini unapokwenda hatua kwa hatua, mwili unazoea na hatimaye mabadiliko makubwa yanatokea.
Kwa kila unachotaka kubadili kwenye maisha yako, kinachokuhusisha wewe binafsi na hata wengine, angalia ni hatua zipi za awali utakazoanza nazo ambazo zitatengeneza mazoea mapya.
Ugumu wa mabadiliko ni kuvunja mazoea ya zamani.
Ukiyavunja moja kwa moja kutatokea upinzani mkali.
Njia bora ni kujenga mazoea mapya kwenye mazoea ya zamani.
Mazoea ambayo hayatofautiani sana na yaliyokuwepo.
Kisha unaenda ukibadili mazoea hayo hatua kwa hatua mpaka unalifikia lengo lako la mabadiliko.
Hili halimaanishi uwe mzembe na uyakimbie mabadiliko kwa sababu ni magumu kwako na kwa wengine.
Mabadiliko lazima yatokee kama mtu unataka kupiga hatua kubwa.
Ni namba ya kusababisha mabadiliko ndiyo inapaswa kuwa ya kimkakati ili usikwame kwenye mabadiliko yako.
Unaweza kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka, lakini yatakuja na gharama zake pia, ambazo zinakuwa kubwa sana.
Gharama hizo zinakuwa binafsi kwa upande wa nguvu, muda na umakini.
Pia gharama hizo zinakuwa kwa wengine kwa kuwapoteza na kupoteza baadhi ya matokeo yaliyokuwepo.
Yote kwa yote, mabadiliko yoyote yale yana gharama ya kulipa.
Ni muhimu sana uhakikishe matokeo unayopata yanaendana na gharama unayolipa kwenye mabadiliko.
Moja ya vitu muhimu kufanya wakati wa mabadiliko ni kuwa na msimamo.
Unapoanza mabadiliko kuna gharama utaingia, ukiona gharama hiyo ni kubwa na kuacha, unakuwa umepoteza gharama ambazo tayari umelipa.
Lakini kama utaendelea na gharama hizo, mwisho utakamilisha mabadiliko ambayo yatakuwa na matokeo makubwa na mazuri.
Tuyaendee mabadiliko yote tunayofanya kwa mkakati sahihi, wa kubadili hatua kwa hatua na kuwa na msimamo hata pale gharama zinapojitokeza.
Mabadiliko siyo rahisi ndiyo maana wengi hawayafanyi.
Wewe jua ugumu wa mabadiliko ulipo na jipange kuukabili ili uweze kuyakamilisha mabadiliko kwa mafanikio makubwa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe