FALSAFA YA KISIMA CHA MAARIFA
Rafiki yangu mpendwa,
Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, jamii ya tofauti kabisa ya watu waliochagua kushika hatamu ya maisha yao.
Huu hapa ni mwongozo wa FALSAFA YA KISIMA CHA MAARIFA, usome na kuuelewa na kisha kuuishi kila siku ya maisha yako.
Karibu sana.
IMANI, MAONO NA MKAKATI WA KISIMA CHA MAARIFA.
Imani kuu ya KISIMA CHA MAARIFA ni UPENDO, upendo ambao unaanzia kwa mtu binafsi kujipenda na kujithamini mwenyewe, kuwapenda wale wote wanaomzunguka na kupenda sana kile anachokifanya na hivyo kukifanya kwa viwango vya juu sana.
Maono makuu ya KISIMA CHA MAARIFA ni kuwa jamii ya tofauti ambayo watu wanachukua jukumu la maisha yao, wanaishi kusudi la maisha yao na kuishi maisha ya mafanikio na furaha.
Mkakati wa kufikia maono hayo ni kupitia kujifunza na kuishi misingi sahihi ya mafanikio, kushirikiana na wengine wenye mtazamo wa mafanikio na kutoa thamani kubwa kwa wengine.
Hivi ni vitu vitatu muhimu sana vya kutupa mwongozo wa namna ya kuishi kama wanamafanikio.
Imani inatufanya tuwe na kitu tunachosimamia na hivyo kutokutetereshwa na mengi yanayopita.
Maono yanatuonesha wapi tunataka kufika kwa pamoja.
Na mkakati unatuonesha tunafikaje kule tunakotaka kufika.
Kwa muda mrefu nimekuwa nashirikisha haya kwa namna mbalimbali, lakini hapa nimeyaweka kwa pamoja kwa njia rahisi kwa kila mtu kuelewa na kuchukua hatua.
IMANI.
Imani yetu kuu ya KISIMA CHA MAARIFA iko wazi, ni UPENDO.
Kama mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA unapaswa kujipenda sana wewe mwenyewe, kujikubali vile ulivyo, kujithamini na kujiheshimu.
Kama mambo hayo hayataanza na wewe mwenyewe, kwa hakika hakuna mwingine anaweza kukupa mambo hayo. Ukijidharau unakuwa umewaruhusu wengine wakudharau. Jipende na jikubali vile ulivyo, ukijua una kila unachohitaji ili uweze kuishi maisha ya mafanikio.
Kuwapenda watu wengine ni kitu kingine muhimu sana kwenye maisha yako ya mafanikio. Chochote unachotaka kwenye maisha yako, kinatoka kwa watu wengine. Ni kupitia kuwapenda na kuwajali wengine ndiyo unaweza kushirikiana nao vizuri na wakawa tayari kukupa kile unachotaka.
Lakini huwezi kuwapenda wengine kama hujajipenda mwenyewe, huwezi kutoa kile ambacho wewe huna. Ndiyo maana ni muhimu uanze kujipenda mwenyewe.
Na unapowapenda wengine, unafanya yale yenye manufaa kwao, huwaumizi au kuwadhulumu kwa namna yoyote ile. Falsafa ya mafanikio tunayoiishi siyo ya jumla sifuri (zero sum) kwamba ili wewe upate lazima mwingine akose, bali ni ya jumla chanya (positive sum) ambapo wewe unaweza kupata na wengine wakapata pia.
Falsafa hii ya mafanikio ni ya kutoa thamani zaidi, tunatoa thamani zaidi kwa wengine ili nao wawe tayari kutupa kile tunachotaka, kwa namna hiyo kila mmoja ananufaika.
Sehemu ya tatu ya upendo ni kupenda kile unachofanya, kila unachoruhusu mikono yako ishike, kipende sana. Kila unachofanya, kifanye kutoka ndani ya moyo wako. Hata kama ni kitu cha chini kabisa, kifanye kwa upendo mkubwa, kifanye kwa kuweka utu wako ndani yake na kwa njia hiyo utaweza kutoa thamani kubwa.
Unapaswa kupenda sana kile unachofanya au kama huwezi kukipenda basi achana nacho mara moja. Kuendelea kufanya usichopenda kwa sababu tu labda kinakupa fedha au heshima fulani ni kujidanganya, huwezi kuwa na mafanikio ya kweli kwenye maisha ambayo yanaambatana na furaha ya kudumu.
Jipende mwenyewe, wapende wengine na penda unachofanya. Huhitaji akili kubwa au elimu ya juu sana kuelewa imani hii, ielewe kwa kina na kuiishi kwenye kila siku ya maisha yako.
MAONO.
Maono ya kuwa jamii tofauti kabisa yanasukumwa na changamoto tunazoziona kwenye jamii. Watu wengi hawapo huru, hawaishi maisha yenye maana kwao, hawana mafanikio na zaidi hawana furaha.
Watu wengi wamewekwa kwenye hali hizo na mamlaka mbalimbali ambazo hazitaki watu wajitambue ili waendelee kuwa chini ya utumwa wao.
Kuanzia kwenye serikali, familia, jamii, dini na mifumo ya elimu, lengo limekuwa ni kujenga jamii ya watu wa kawaida ili waweze kutawaliwa.
Jamii ya KISIMA CHA MAARIFA ni ya tofauti, ni ya watu wanaojitambua, wanaojua kusudi la wao kuwa hapa duniani, waliochukua jukumu la kuyajenga maisha yao badala ya kutoa jukumu hilo kwa wengine na inayoishi maisha ya mafanikio na furaha.
Hayo ni mambo yanayowezekana kama mtu atachagua kuishi kwa Falsafa hii ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kuwa kwenye jamii hii husubiri wengine wakuchague na kukuambia unafaa kwa kitu fulani, unajichagua wewe mwenyewe na kuhakikisha unafaa kwa namna unayotaka.
Kwa kuwa kwenye jamii hii hulaumu wengine au hali zozote zile kwa kuwa sababu ya maisha yako kutokuwa unavyotaka. Badala yake unajua hilo ni jukumu lako na kuchukua hatua sahihi.
Kwa kuwa kwenye jamii hii huwalalamikii wengine pale unapokosa kile unachotaka au kwa mambo wanayofanya, unawaacha watu wahangaike na mambo yao na wewe kuhangaika na mambo yako.
Uhuru ndiyo kitu kikubwa tunachopigania kwenye jamii hii na unaanza na uhuru wa kifedha, uhuru wa muda, uhuru wa maisha. Uhuru ndiyo unafanya mtu awe na mafanikio na kuwa na furaha pia.
Kila maamuzi tunayofanya tunaangalia kwanza uhuru wetu, maamuzi hayo yatupe uhuru zaidi kuliko kupunguza uhuru wetu.
MKAKATI.
Mkakati wa kuyafikia maono ya KISIMA CHA MAARIFA ni kupitia kujifunza na kuishi misingi sahihi ya mafanikio. Tunajua yapo mengi ambayo hatuyajui na hatuwezi kumaliza yote tunayopaswa kuyajua kwenye maisha yetu, hivyo tumechagua kujifunza kwenye kila siku ya maisha yetu na kuyaboresha maisha yetu kupitia yale tunayojifunza.
Tunajua pia kwamba hatuwezi kufanya kila kitu peke yetu, tunahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wengine. Hivyo mkakati wetu unahusisha kushirikiana na wengine, hasa wale wenye mtazamo wa mafanikio kama sisi, ili kwa pamoja tuweze kupiga hatua kubwa kwa pamoja na kwa mmoja mmoja.
Kikubwa kabisa kwenye mkakati wetu wa mafanikio ni kutoa thamani kubwa mno kwa wengine kupitia kila tunachofanya na jinsi tunavyoyaishi maisha yetu. Tunajua tunaweza kupata chochote kile tunachotaka, kama tutawasaidia wengine wengi kupata kile wanachotaka. Hivyo kwa kila tunachofanya, tunaangalia tunawanufaishaje wengine na siyo kuangalia sisi tunanufaikaje pekee.
MSINGI, MWONGOZO NA MSIMAMO WA KISIMA CHA MAARIFA.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA tuna MSINGI, MWONGOZO na MSIMAMO tunavyotumia katika kufanya maamuzi yetu mbalimbali na kuchukua hatua za kimafanikio.
MSINGI
Msingi wa KISIMA CHA MAARIFA ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA.
Jiwe kuu kabisa la mafanikio yetu limejengwa kwenye NIDHAMU, ambayo ni kupanga na kufanya kama ambavyo mtu umepanga. Nidhamu ndiyo kipimo na msukumo wako wa ndani wa mafanikio.
Kuna nidhamu mbalimbali ambazo tunapaswa kuziishi kila siku.
Nidhamu binafsi ya kupanga na kufanya kama ulivyopanga bila kuahirisha.
Nidhamu ya fedha kwa kuhakikisha matumizi hayazidi kipato, unaweka akiba kwenye kila kipato na kuwekeza akiba hiyo maeneo ambayo inazalisha faida na kukua thamani.
Nidhamu ya muda ambapo unapangilia muda wako na kuutumia vizuri bila ya kuupoteza.
Nidhamu ya kazi ambapo unajiwekea viwango vya juu kwenye kila unachofanya na kujisukuma kuvifikia.
Nidhamu ya mahusiano ambapo unaboresha mahusiano yako kupitia kuyapa muda na kuwajali wengine.
Uadilifu ni kitu kinachojenga na kulinda mafanikio. Unaweza kufanikiwa kwa njia zisizo sahihi, lakini mafanikio hayo hayawezi kudumu, ushahidi upo wazi kwenye hili.
Hivyo tunakuwa waadilifu sana kwenye maisha yetu, tunafanya yale yaliyo sahihi, tunatekeleza yale tunayoahidi na tunawatendea wengine yale ambayo tungependa watutendee sisi pia.
Kwa uadilifu, unakuwa na maisha ya aina moja tu, faraghani na hadharani. Huwi na mambo unayoficha kwenye maisha yako na hivyo hakuna yeyote anayeweza kukuhujumu.
Kwa uadilifu, maisha yako yanakuwa rahisi na yanayoeleweka kwako na kwa wengine, kitu kitakachofanya nguvu zako zote utumie kwenye mafanikio badala ya kuficha vitu au kukazana kujielezea kwa wengine.
Kujituma ni kwenda hatua ya ziada kwa kila tunachofanya, kuwashangaza watu kwa kufanya zaidi ya walivyotegemea.
Kujituma kunatufanya tupige hatua kubwa na kupata matokeo ya tofauti kwa kila tunachofanya.
Kujituma kunayavunja mazoea ambayo ndiyo kifo cha mafanikio ya wengi.
Kwa kujituma kwenye kila jambo, tunajifunza na kufanya vitu vya tofauti na hivyo kuwa mbele zaidi kimafanikio.
Msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ni msingi tunaouishi kila siku bila ya kuuvunja kwa kuwa mafanikio yetu yanajengwa hapo na kulindwa pia.
Ukiishi msingi huo ukapata mafanikio halafu ukaacha kuuishi, mafanikio yote uliyojenga yanavunjika.
MWONGOZO
Mwongozo wa mafanikio ni njia ya kuweka vipaumbele katika yale ambayo mtu unayafanya.
Dunia ya sasa ina mafuriko ya taarifa na fursa mbalimbali, kama huna chujio la kuweka vipaumbele vyako, utahangaika na mengi na mwisho hutaona matokeo ya tofauti uliyopata.
Mwongozo wa KISIMA CHA MAARIFA unajenga na vitu vitatu; AFYA, HEKIMA NA UTAJIRI.
Kwenye afya, hiki ni kipaumbele cha kwanza, kuhakikisha afya inakuwa bora na imara kwa kuwa afya ndiyo mtaji wa kwanza. Hapa inahusisha afya ya akili, mwili na roho.
Kwenye afya kuna mambo matatu muhimu ya kuzingatia ambayo ni kula kwa usahihi, kufanya mazoezi ya mwili na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.
Kitu muhimu sana kwenye afya ni kinga ni bora kuliko tiba, ukiyazuia magonjwa yasitokee unakuwa kwenye nafasi nzuri kuliko kupambana na magonjwa yakishatokea.
Kwa kufanyia kazi kipaumbele cha afya, tunajiweka kwenye njia nzuri ya kufanikiwa.
Hekima ni kipaumbele kingine muhimu kwenye mafanikio yetu. Mafanikio tunayopata kwenye maisha ni matokeo ya ukuaji wetu binafsi. Kama hukui, huwezi kufanikiwa.
Njia pekee ya kukua binafsi ni kuendelea kujifunza na kuyaishi yale unayojifunza, na hiyo ndiyo hekima.
Kuna watu wanajua mambo mengi, lakini kama hawayaishi yale wanayoyajua hawana hekima. Daktari anaweza kujua uvutaji wa sigara unasababisha saratani nyingi kwenye mwili wa mwanadamu, lakini bado akavuta sigara. Anachokosa daktari huyo siyo elimu bali hekima.
Kipaumbele chetu kwenye KISIMA CHA MAARIFA siyo tu kupata elimu na maarifa, bali kuyaishi maarifa hayo, kuyafanya sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hiyo ndiyo hekima na hivyo ndivyo mtu unaweza kufanikiwa, siyo kwa kujua, bali kwa kuweka kwenye matendo yale unayoyajua.
Utajiri ni kipaumbele kingine muhimu tunachokitumia kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Tunajua fedha ni muhimu kwa mambo yote yanayohusu fedha na fedha ndiyo inayonunua uhuru wetu.
Hivyo tunaupenda utajiri, na tunafanyia kazi kuwa nao kwenye maisha. Hatusemi utajiri ni mbaya au haununui furaha. Tunajua utajiri ni mzuri, kwa sababu unatuwezesha kuishi maisha yetu kwa namna tunavyotaka, lakini pia unatuwezesha kuwasaidia wengine wenye uhitaji.
Tunajua njia bora ya kuwasaidia masikini siyo kuwa masikini kama wao na kuwafariji kwamba utajiri siyo mzuri, bali kwa kutokuwa masikini kama wao na kuwasaidia kufikia utajiri kama ambao umefikia.
Katika kujenga utajiri tunazingatia kuongeza kipato, kuweka akiba na kuwekeza akiba zetu kwenye maeneo yanayoifanya izalishe zaidi. Tunajua utajiri haujengwi kwa kipato pekee, bali kwa uwekezaji sahihi unaofanywa kwa muda mrefu.
Mwongozo huu wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA ndiyo tunautumia kwenye maamuzi yote muhimu tunayofanya na jinsi tunavyoyaishi maisha yetu.
MSIMAMO
Msimamo wa KISIMA CHA MAARIFA ni namna tunavyofanya mambo yetu, namna tunavyoacha alama kwa kila tunachofanya.
Msimamo huo ndiyo unaotutambulisha kwa wengine, unaowafanya watuamini na kututegemea kwa sababu hatuyumbi kwenye msimamo huo.
Msimamo wa KISIMA CHA MAARIFA unajenga na mambo matatu, KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kazi ni kipaumbele kikubwa kwetu, tunaipenda kazi kwa kuna ndiyo njia yetu ya kugusa maisha ya wengine. Hivyo tunaweka viwango vikubwa kwenye kazi zetu na kujisukuma kuvifikia. Kila tunachogusa, kuna alama tunayoiacha ambayo wengine wanajua ni sisi tumefanya kazi hiyo.
Upendo ndiyo imani yetu kuu na hakuna kinachotuyumbisha kwenye hilo.
Huduma ni lengo la kila kazi tunayofanya, kuwahudumia wengine, kufanya maisha yao kuwa bora kuliko yalivyokuwa awali. Kuacha alama fulani kwenye maisha yao ambayo imetokana na kazi zetu.
Maisha yetu ni ya huduma kwa wengine, tunaishi siyo kwa manufaa yetu tu, bali kwa manufaa ya wengine pia.
Kwa msimamo wa KAZI, UPENDO NA HUDUMA, wengine wanatuamini na kututegemea, kwa kujua tutafanya kilicho sahihi mara zote.
KLABU ZA KISIMA CHA MAARIFA.
Tumeona mkakati wa kufikia maono ya KISIMA CHA MAARIFA ni kupitia kushirikiana na wengine wenye mtazamo wa mafanikio kama sisi.
Tunafanya hivyo kupitia KLABU ZA KISIMA CHA MAARIFA, ambapo ni mkusanyiko wa wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA walio kwenye mkoa mmoja.
Klabu hizi zina lengo kuu la kuwaleta wanachama pamoja na kushirikiana katika kuyafikia maono ya KISIMA CHA MAARIFA.
Lakini pia klabu zina wajibu wa kuisaidia jamii kwa ujumla katika maeneo mbalimbali, ikiwepo kutoa elimu ya mafanikio, kutoa misaada kwa wenye uhitaji na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.
Ili kuwaleta wanamafanikio pamoja na kushirikiana kwa karibu, klabu inakuwa na shughuli ya kiuchumi ya pamoja kama biashara, kilimo au uwekezaji.
Klabu inakuwa na mikutano ya wanachama wote kukutana angalau mara moja kila mwezi.
Kupitia klabu za KISIMA CHA MAARIFA, kila mwanachama anapata nafasi ya kushirikiana na wengine na kusukumwa kuyafikia malengo yake na yale ya klabu pia.
WAJIBU WA MWANACHAMA WA KISIMA CHA MAARIFA.
Kila maono makubwa yana wajibu mkubwa kwa kila anayeshiriki ili yaweze kufikiwa. Maono hayatatokea yenyewe, yatatokana na juhudi ambazo kila mtu anaweka.
Kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA atakuwa na wajibu ufuatao katika kuhakikisha maono ya KISIMA CHA MAARIFA yanafikiwa.
- Kulipa ada ya KISIMA CHA MAARIFA na ya KLABU YA KISIMA CHA MAARIFA ambayo yupo ili kuhakikisha huduma hii inaendelea bila ya kikwazo chochote.
- Kuishi kwa imani, msingi, mwongozo na msimamo wa KISIMA CHA MAARIFA kwenye maisha ya kila siku. Kiashiria cha kama anaishi hayo kitaonekana kwenye matokeo anayozalisha kwenye maisha yake.
- Kuwa mwanachama hai wa KLABU YA KISIMA CHA MAARIFA ambapo yupo kwa kuhudhuria mikutano na kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za klabu.
- Kuwa na malengo makubwa ambayo anayafanyia kazi kila siku na kujifanyia tathmini kila mwezi ambayo anamshirikisha Kocha.
- Kuwa balozi mzuri wa KISIMA CHA MAARIFA popote anapokuwa kwa kujitofautisha na wengine wasioishi kwa msingi na falsafa ya KISIMA CHA MAARIFA. Kutumia nafasi hiyo kuwaalika wengine kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
- Kushiriki MKUTANO MKUU WA KISIMA CHA MAARIFA ambao unafanyika mara moja kila mwaka na kuwaleta wanamafanikio wote pamoja katika kujifunza na kushirikishana hatua za mafanikio wanazopiga.
- Kujijengea uhuru wa kifedha na utajiri kupitia kuwa na vyanzo vingi vya kipato, kuweka akiba na kufanya uwekezaji ambao unazalisha faida na kukua thamani. Muhimu pia ni mwanachama kuwa na biashara anayoiendesha kwa mfumo ambayo haimtegemei moja kwa moja.
- Kuendelea kujifunza na kujiendeleza binafsi na kile anachofanya.
- Siku moja kuandika kitabu cha maisha yako au uzoefu ambao umekutana nao kwenye maisha na hatua ulizopiga ili kuwasaidia wengine kujifunza kutokana na maisha yako.
- Kuiishi falsafa ya KISIMA CHA MAARIFA kwa hiari yake mwenyewe na siyo kwa kusukumwa au kulazimishwa na mtu yeyote. Na hapa kujitoa kweli kuhakikisha anafikia mafanikio makubwa kwenye maisha.
Kwa kila mwanachama kutimiza wajibu wake, itapelekea maisha yake kuwa bora na falsafa ya KISIMA CHA MAARIFA kuwa na matokeo mazuri kwa wote.
WAJIBU WA KOCHA.
Kocha ambaye ni mwasisi na kiongozi wa KISIMA CHA MAARIFA anawajibika kuhakikisha kila mwanachama anaishi falsafa hii ya mafanikio na kupata matokeo mazuri kwenye maisha yake, yaani kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha.
Katika kuhakikisha kila mwanachama anafanikiwa, Kocha anawajibika kama ifuatavyo;
- Kushirikiana na kila mwanachama kwa ukaribu, kujua ndoto anazotaka kufikia, hatua anazochukua, changamoto anazopitia na matokeo anayopata.
- Kumshauri na kumwongoza vyema kila mwanachama katika kuishi falsafa hii na kufikia mafanikio kwenye maisha.
- Kumwongoza kila mwanamafanikio kujenga mfumo wa biashara inayojiendesha yenyewe bila kumtegemea moja kwa moja.
- Kutembelea klabu za KISIMA CHA MAARIFA na kusaidia ukuaji wake pamoja na kushirikiana nazo kwa karibu.
- Kuwatembelea wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kwenye biashara zao na hata familia zao pale inapohitajika kufanya hivyo.
- Kuendelea kutoa mafunzo ya mafanikio kwa njia mbalimbali.
- Kupokea tathmini za mwezi za kila mwanachama na kushauri hatua za kuchukua kulingana na yale ambayo mtu anapitia.
- Kumsimamia kila mwanachama ili kuhakikisha anafanikiwa na kutokumruhusu ajipe sababu mbalimbali.
- Kuendesha MIKUTANO MIKUU YA MWAKA YA KISIMA CHA MAARIFA kila mwaka.
- Kusimamia imani, maono na mkakati wa KISIMA CHA MAARIFA na kuendelea kuja na ubunifu wa kuboresha falsafa ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa Kocha kutimiza wajibu wake, ataiwezesha falsafa ya KISIMA CHA MAARIFA kuendelea kuwa hai na watu kunufaika nayo kwa kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.
MAMBO YA NYONGEZA.
Ni imani yangu umeielewa vizuri falsafa hii, hakuna jipya hapa, yote nimekuwa nayashirikisha kwa njia mbalimbali.
Nilichofanya hapa ni kuyarahisisha kwa kuweka pamoja yale muhimu ambayo ndiyo yanaijenga falsafa hii ya mafanikio kwa namna ambayo mtu unaweza kuielewa na kuiishi.
Hapa kuna mambo muhimu ambayo ningependa kuyatolea ufafanuzi zaidi ili yaeleweke na yaweze kufanyiwa kazi na kila anayehusika.
FAMILIA
Tulipoanza KISIMA CHA MAARIFA, mtu alikuwa anajiunga yeye binafsi kuwa mwanachama. Lakini kadiri tunavyokwenda nimekuwa naona hitaji la watu kwenye familia ya wanachama kutaka kunufaika pia na KISIMA CHA MAARIFA.
Pia wakati mwingine uanachama wa mtu unaleta changamoto kwa wanafamilia wengine, hasa wenza. Mfano kwa wanachama ambao ni wanawake na wameolewa, baadhi wamekuwa wanapata changamoto kwa waume zao kutokukubaliana nao pale wanapohitaji kushiriki mambo mbalimbali ya KISIMA CHA MAARIFA kama klabu na mikutano ya mwaka.
Nimeona pia wanachama wakiwaleta watu wengine kwenye familia ili wapate huduma mbalimbali.
Hivyo natoa nafasi ya uanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kuwa unahusisha familia nzima. Kama utapenda mwenza wako, yaani mke au mume naye awe mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, basi nafasi hiyo ipo.
Hili siyo lazima, ila ni fursa kwa wale ambao wenza wao au watoto wao wanahitaji kutumia KISIMA CHA MAARIFA katika kupiga hatua kwenye maisha yao.
Na kwa kuwa hii ni falsafa ambayo tunaiamini ni sahihi na kuiishi, kwa nini pia usiijenge kwenye familia yako?
Hivyo mwanachama anaweza kushiriki na familia yake kwenye shughuli mbalimbali za KISIMA CHA MAARIFA kama klabu, mikutano ya mwaka na kupata huduma nyingine za Kocha.
HAMASA
Kuna watu ambao bado wanataka hamasa ya kila mara ndiyo waweze kupiga hatua. Mwanzo wanapoanza kitu wanakuwa na hamasa kubwa na kujituma sana, mpaka hata kupitiliza. Lakini baadaye hamasa hiyo inakuwa imeisha na hawafanyi tena.
Falsafa hii inahitaji kujitoa na kujenga mfumo wa kuyaendesha maisha yako ambao utaufuata kila siku na siyo kusubiri mpaka upate hamasa.
Unapochagua kuiishi falsafa hii maana yake umeachana na ile hali ya kusukumwa na hamasa za nje, umejitoa ndani yako kwamba lazima ufanikiwe.
Hivyo nikutake usije kwangu kila mara ukitaka hamasa, bali njoo kwangu na changamoto, ili tushirikiane kuitatua na kusonga mbele.
Ninachoka sana pale mtu anapotaka nimhamasishe kila siku, pale mtu anakuja na sababu zile zile kila siku.
Ninachotaka kutoka kwa kila mwanachama sasa ni kuja na changamoto, kuniambia nimechukua hatua hii na nimekutana na changamoto hii, nifanyeje ili kutoka hapa.
Hapo sasa ndiyo tunafanya kazi pamoja kuhakikisha unaivuka changamoto na kupiga hatua.
UBOBEZI
Kwa chochote unachofanya, iwe ni kazi ya kitaaluma au biashara, unapaswa kujenga ubobezi.
Hivyo unapaswa kuchukua kozi mbalimbali za kubobea kwenye mambo unayofanyia kazi.
Kama unaweza kujiendeleza kielimu kwa mfumo rasmi wa elimu ni vizuri, ila fanya hivyo kwa lengo la kupata ujuzi zaidi utakaoutumia kwenye safari ya mafanikio, na siyo kutaka tu upate sifa za juu za kielimu.
Kama hutaki kutumia njia rasmi basi tumia mtandao wa intaneti kujifunza kozi zinazoendana na kile unachofanya. Vyuo mbalimbali duniani vinatoa elimu nzuri kwa njia ya mtandao, kwa gharama rahisi au hata bure kabisa.
Hivyo kuwa na mkakati wa kujijengea ubobezi kwa kusoma kozi mbalimbali mtandaoni.
Sehemu nzuri ya kuanzia ni kwenye mtandao wa COURSERA; www.coursera.org Ingia kwenye mtandao huo, tengeneza akaunti yako na anza kuchukua kozi mbalimbali kulingana na mpango wako wa ubobezi.
Kwa kila kozi unayokamilisha utapewa cheti na hicho utakituma kwa Kocha kama sehemu ya ushahidi kwamba unafanyia kazi mpango wa ubobezi.
KUJIFUNZA
Kuendelea kujifunza hasa kupitia usomaji wa vitabu ni hitaji muhimu unalopaswa kuendelea kulifanyia kazi kila siku.
Kwa kiwango cha chini kabisa, soma kitabu kimoja kila mwezi. Usikubali mwezi uishe hujasoma kitabu chochote kile.
Ukiweza kusoma zaidi ya hapo ni vizuri sana, lakini usikubali sababu yoyote ikuzuie kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi.
MFUMO WA BIASHARA
Moja ya majukumu ya kocha ni kuhakikisha kila mwanachama anajenga biashara yenye mfumo wa kuiwezesha kujiendesha yenyewe.
Hili ndilo eneo kubwa sana ambalo naona linaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa kila mmoja, kuanzia mtu binafsi mpaka vizazi vyake.
Biashara za wengi hazina mifumo, zinawategemea wao binafsi kitu kinachoziweka kwenye hatari.
Tumeona kwenye jamii, watu wengi wanapofariki biashara zao nazo zinakufa na watoto wao kulazimika kuanzia sifuri.
Hili halipaswi kutokea kwa wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, kila mmoja wetu anapaswa kujenga biashara inayojiendesha kwa mfumo, ili hata anapokuwa hayupo, biashara iendelee kwenda na ifaidishe vizazi na vizazi.
Watoto na watu wengine wa karibu wajue misingi ya biashara na kuiheshimu ili wasiiue pale inapokuwa kwenye mikono yao.
Hivyo hapa natoa nafasi kwa kila mwanachama kutumia fursa hii vizuri, tushirikiane katika kutekeleza hili ili liwe na manufaa kwetu na vizazi vyetu.
KUONGEZA WANACHAMA
Njia kuu niliyokuwa natumia awali kuongeza wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA ni kupitia kuwashawishi wale wanaopata kazi zangu nyingine kujiunga. Njia hiyo itaendelea kutumika, hasa pale watu wanapotaka zaidi.
Lakini njia ambayo itafanyiwa kazi zaidi ni mwanachama kuleta mtu mwingine. Hapa kila mwanachama ana nafasi ya kuwakaribisha wengine wajiunge na KISIMA CHA MAARIFA.
Na ndiyo maana ni muhimu kila mwanachama kuiishi Falsafa hii ya KISIMA CHA MAARIFA kwa uhalisia ili azalishe matokeo ya tofauti na wale wanaomzunguka watamani kuwa kama yeye na hapo awakaribishe kujiunga.
Unapomkaribisha mtu na akajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, wewe ndiye unakuwa mlezi (menta) wake kwa siku za mwanzo kwenye KISIMA, kumsaidia aweze kuiishi falsafa hii pia.
KUWASILIANA NA KOCHA
Kwa kila mwanachama, una nafasi ya kuwasiliana na kocha kwa jambo lolote na kwa muda wowote. Kama ni kwa njia ya ujumbe unaweza kutuma email kwenda kochamakirita@gmail.com au kwa wasap +255 717 396 253
Kama ni jambo linalohitaji maongezi ya simu au kukutana ana kwa ana, unatuma ujumbe kwa njia hizo kisha tunapanga kufanya hivyo.
Ninatoa nafasi zaidi kwa kila mwenye uhitaji na nashauri sana kwa kila maamuzi makubwa unayoyafanya unishirikishe ili tusaidiane yaweze kuwa maamuzi bora zaidi.
Milango ya mawasiliano iko wazi, itumie.
KUFUTWA UANACHAMA
Wajibu namba 10 wa kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA ni kuchagua kuwa mwanachama kwa hiari yako mwenyewe. Kwa sababu umeona ni kitu chenye manufaa kwako, lakini pia umejitoa kuishi kulingana na misingi hii na kutekeleza wajibu wako.
Hakuna atakayekulazimisha kwa namna yoyote ile uwe mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, ni kitu kinachopaswa kutoka ndani yako.
Hakuna atakayesikiliza sababu yoyote unayotoa kwa nini umeshindwa kuishi kwa misingi au kutekeleza wajibu wako kama mwanachama. Huishi hivi kumridhisha yeyote bali kwa kuchagua mwenyewe.
Hivyo uanachama wa KISIMA CHA MAARIFA utafutwa katika hali hizi mbili;
Moja ni mtu mwenyewe kuamua kwamba hataki tena kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA.
Mbili ni mtu anaposhindwa kuishi kwa falsafa hii, anapoenda kinyume na imani, msingi, mwongozo na msimamo na anapoacha kutekeleza wajibu wake kama mwanachama.
NATAKA KUENDELEA KUJIFUNZA LAKINI SITAKI KUBANWA NA FALSAFA HII.
Kuna ambao wamekuwa wakieleza kwamba wanataka kuendelea kujifunza kupitia KISIMA CHA MAARIFA ila hawataki kubanwa na falsafa hii, wao wanajifunza tu na kuchagua kuishi kwa falsafa zao nyingine walizonazo na siyo hii ya KISIMA CHA MAARIFA.
Jibu ni kwamba nafasi hiyo haipo tena kwenye KISIMA CHA MAARIFA, zipo njia nyingine unazoweza kujifunza kupitia maarifa ninayotoa na nitaziorodhesha hapo chini. Endelea kuzitumia na utanufaika na mengi.
Kwenye KISIMA, hata kama upo tayari kulipa ada, hiyo tu haitoshi kukupa uanachama. Kama ambavyo nimekuwa naeleza, ada ninayotoza kwenye huduma ya KISIMA CHA MAARIFA ni ndogo kuliko thamani unayoipata.
Nafanya hivyo makusudi kabisa, kwa sababu nawekeza kwako, najua ukiishi misingi hii na maisha yako yakabadilika, wengine watataka kujua siri yako, utawaleta kwenye KISIMA CHA MAARIFA na wao kuwa wanachama pia, hapo tunaikuza zaidi jamii hii.
Lakini kujifunza tu utakavyo na kutokuyaishi haya, unakuwa unaniibia, unakuwa unanitumikisha mimi kukupa thamani kubwa huku wewe huleti thamani hiyo.
Lakini pia unajaza nafasi ambazo wengine wangeweza kuzitumia vizuri.
Hivyo kama nilivyosema, uanachama wa KISIMA CHA MAARIFA ni wa hiari kabisa, hakuna kulazimishwa kwa namna yoyote ile, hakuna kutishwa kwamba usipokuwa mwanachama basi maisha yako hayatakuwa mazuri.
Nikuhakikishie tu, unaweza kufanikiwa kwenye maisha yako iwe upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA au haupo. Hivyo ninachotaka ni watu walioielewa falsafa hii, watu ambao wameipenda na wapo tayari kuiishi kwenye maisha yao, kisha tuambatane kwenye safari hii kwa maisha yetu yote.
Kwa uzoefu niliopata kwenye kuendesha huduma hizi ni kwamba huwezi kumbadilisha mtu. Hivyo sihangaiki kumbadilisha yeyote, bali nakazana kuwavuta wale walio sahihi, wale wanaoilewa falsafa hii.
Hivyo kama umeisoma falsafa hii na kuielewa, kama ndani yako umesikia sauti ya hiki ndiyo ninachotaka, basi karibu twende pamoja.
Kama ndani yako umeona ni kitu cha ajabu, kama umeona hutaki yeyote akupangie namna ya kuishi, uko huru kuchagua kitu kingine.
Watu wote kwenye jamii hawajawahi kukubaliana kwenye kitu kimoja. Mungu ni mmoja lakini dini ni nyingi. Biblia na Yesu ni mmoja lakini madhehebu ni mengi. Kadhalika mafanikio kwenye maisha ni kitu kimoja lakini zipo njia na mifumo mbalimbali ya kufikia.
Mfumo wetu wa KISIMA CHA MAARIFA ni moja ya hayo, kama umeuelewa na umeukubali, karibu sana.
Kwa kuwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA ninaamini utakuwa umekomaa kuweza kuupokea ukweli jinsi ulivyo. Na hivyo kila nitakachokuwa nakuambia kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni kweli kama ilivyo, bila kujali kama inakuumiza au la. Kwa sababu najua huwezi kukua kama hutakuwa tayari kuukabili ukweli mchungu.
Chagua hii leo kama hii ni falsafa unayotaka kuendesha nayo maisha yako yote, kisha fanya maamuzi sahihi.
Nimechagua kuifanyia kazi falsafa hii ya KISIMA CHA MAARIFA kwa kipindi chote cha maisha yangu na hivyo nakaribisha wote ambao wamejitoa kwa ajili ya falsafa hii twende pamoja.
Sitamuacha yeyote nyuma ambaye amejitoa kweli kwenda na falsafa hii, haijalishi ameanzia wapi au anaanguka mara ngapi. Kama utaiishi falsafa hii, niko pamoja na wewe na nina hakika utafanikiwa na kudumu kwenye mafanikio. Ni swala la muda tu.
NJIA MBADALA ZA KUJIFUNZA
Zifuatazo ni njia mbadala za kujifunza kupitia maarifa na huduma mbalimbali ninazotoa.
- Makala za maisha na mafanikio; www.amkamtanzania.com
- Uchambuzi wa vitabu mbalimbali; https://www.t.me/somavitabutanzania
- Vitabu mbalimbali nilivyoandika na kuchapa (hardcopy); www.somavitabu.co.tz
- Vitabu mbalimbali nilivyoandika kwa mfumo wa nakala tete; https://play.google.com/store/apps/details?id=somavitabu.co.tz.somakitabu au ingia PLAY STORE na tafuta SOMA VITABU.
HITIMISHO.
Ni imani yangu umeielewa vizuri falsafa hii ya KISIMA CHA MAARIFA.
Na ni imani yangu kwamba utafanya uchaguzi sahihi katika hili.
Kama kuna ambapo hujaelewa vizuri, unaweza kuwasiliana na mimi muda wowote nikakupa ufafanuzi zaidi.
Pia kama una mapendekezo ya kuboresha zaidi falsafa hii ili iweze kuzalisha matokeo bora kwa kila mmoja wetu, nakukaribisha ushirikishe pia.
Rafiki yako katika kuiishi falsafa ya KISIMA CHA MAARIFA,
Kocha Dr. Makirita Amani.